NEC: Hatuna mgombea aliyejitoa mbio za urais

20Oct 2020
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
NEC: Hatuna mgombea aliyejitoa mbio za urais

​​​​​​​TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haina taarifa wala haijapokea maelezo  rasmi ya kuwapo mgombea wa urais wa Muungano, aliyejitoa kushiriki uchaguzi mkuu wiki ijayo.

Akizungumza na wadau wa uchaguzi Visiwani Zanzibar, Kamishna wa NEC, Hasina Omar alisema kutofanya kampeni kwa baadhi ya wagombea wa urais hakuwaondolei sifa ya ugombea kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Jumatano ijayo.

NEC imepitisha wagombea 17 kati ya 19 walioomba kuteuliwa nafasi hiyo ambao watapigiwa kura katika uchaguzi mkuu huo.

Alisema vyama vilivyoteuliwa ni pamoja na AAFP, ACT Wazalendo, ADA TADEA, ADC, CCM ,CCK, CHADEMA, CHAUMMA, Chama cha Wananchi CUF, DP, Demokrasia Makini, NRA, NCCR Mageuzi, SAU, UMD na UPDP.

Alibainisha kwamba NEC imeteua wagombea urais na makamu wao kutoka vyama 15 vya siasa ambapo katika uteuzi huo wanawake wawili walijitokeza na kuteuliwa kugombea kiti cha urais wakati watano wanagombea nafasi ya makamu wa urais.

Alisema kutokana na hali hiyo NEC imepitisha wagombea wote na watakuwamo katika karatasi ya kupigia kura Jumatano ijayo.

Alieleza kwamba ni mara ya kwanza kwa Tanzania vyama vingi vya siasa kusimamisha wagombea wa kiti cha urais hali ambayo inaashiria kukua kwa demokrasia.

Mkurugenzi wa NEC,  upande wa Zanzibar, Hamidu Mwanga, alisema kwa mujibu wa katiba ya Tanzania ibara ya 74 (6) tume  inasimamia na kuratibu uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.

Hivyo, aliwahakikishia wananchi kuwa NEC itasimamia uchaguzi huo kwa kufuata katiba, sheria na miongozo ili uwe wa  uwazi, uhuru na haki.

Akizungumzia utoaji wa matokeo siku ya uchaguzi alisema ni kosa la jinai kwa mgombea kutangaza matokeo na kazi hiyo inafanywa na tume pekee hivyo aliwasisitiza kujiepusha na kosa hilo.

Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi wiki ijayo Oktoba 28, kutumia haki yao kikatiba na pale wanapomaliza kupiga kura kurudi nyumbani kusubiri matokeo.

Habari Kubwa