NEC kutoa barua za mawakala kesho

26Oct 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
NEC kutoa barua za mawakala kesho

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema imepanga kutoa barua za utambulisho wa mawakala kesho.

Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Charles, AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI JANA.

Vile vile, imesema haijapokea taarifa rasmi kutoka kwa wasimamizi wa majimbo kuhusu vyama kulalamika baadhi ya mawakala wake kutoapishwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Charles, alikiri kuwa mawakala hao hawajapewa barua na kuahidi kutolewa kesho (Oktoba 27).

“Mawakala hawajapewa barua kwa kuwa tumepanga zitatolewa Oktoba 27, kwa hiyo zipo kwenye maandalizi, kinachotaka kutokea ni baadhi ya vyama havitaki kufuata taratibu zilizowekwa. Wasimamizi wa uchaguzi ndani ya majimbo tutasikitika sana kama umemwapisha mtu halafu huandai barua yake,” alisema.

“Wakumbuke masuala ya kisheria yapo, na ukifanya mambo ya ovyo sio mwisho, haki nyingine zitatafutwa kwa hatua nyingine ni vyema mkazingatia utaratibu.”

Kadhalika, Mkurugenzi huyo wa NEC, alisisitiza kuwa matokeo yatatangazwa kwa wakati baada ya watu kumaliza kupiga kura.

 

Kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya mawakala hawajaapishwa, alisema: “Hatujapokea taarifa rasmi kwa wasimamizi wa majimbo kuhusu vyama kulalamika baadhi ya mawakala wake kutoapishwa, kuna maeneo tulipigiwa simu na tukashughulikia.”

Akizungumzia kampeni, alisema kwa upande wa Tanzania Bara zitahitimishwa Oktoba 27, wakati Zanzibar wanahitimisha leo.

“Sasa hivi tuna ratiba ya toleo la sita ambalo ndio la mwisho, kwa hiyo tunataka kusisitiza ratiba hiyo inaangalia maadili ya uchaguzi ya mwaka 2020 kwamba kampeni zinaanza saa mbili asubuhi na kuisha saa 12 jioni,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuna tatizo la baadhi ya vyama au wagombea kutozingatia muda licha ya kuelezwa, lakini wamekuwa wakaidi.

“Kumekuwa na tatizo kwa baadhi ya vyama kuwazuia wagombea urais wanaopita huko, unakuta mgombea ubunge au diwani anakuwa na mkutano eneo ambalo mgombea urais anapita. Kama mgombea ana mkutano kwenye eneo hilo msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo anatakiwa kusimamisha mikutano ya kampeni kwa wagombea ubunge na udiwani,” alisisitiza.

Kadhalika, alisema hakuna nafasi ya kubadili ratiba hiyo na kuwataka wagombea kufuata iliyotolewa kwenye maeneo waliyoamua wenyewe na wazingatie kumaliza saa 12 jioni.

“Wanaosaidia kuratibu kampeni hizo ngazi ya jimbo, waache wagombea wa kiti cha urais na makamu wa rais wafanye kampeni zao kwa amani, kama mgombea anafuata ratiba toleo la sita ukienda nje ya hiyo ndio utakapokumbana na tatizo, usivamie eneo ambalo sio la kwako,” alisema.

Akizungumzia vifaa vya kupigia kura, aliwahakikishia Watanzania kuwa Tume imejiandaa vizuri na vifaa vyote muhimu hadi jana jioni vilikuwa vimefika kwenye majimbo yote nchini.

“Na kule jimboni wasimamizi wa uchaguzi wamejipanga vizuri, na sasa wamejipanga kuvisafirisha kupeleka kata na vituo husika, tunawasihi watumie siku ya leo na kesho kutwa kufikisha kwenye vituo ili kusiwe na tatizo la kuchelewesha vifaa,” alisema.

Alisisitiza kuwa hakutakuwa na tatizo la vituo vya kupigia kura kuchelewa kufunguliwa saa moja asubuhi siku ya Oktoba 28 na kuwasihi Watanzania wajitokeze ili kupiga kura.

Kwa upande wa vitambulisho, alisisitiza kuwa mpigakura aliyejiandikisha na kupoteza kadi atapiga kwa kitambulisho mbadala vilivyoainishwa na Tume baada ya kuthibitisha kuwa amepoteza.

Habari Kubwa