NEC: Waangalizi wasiwe wasemaji wa uchaguzi

18Oct 2020
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
NEC: Waangalizi wasiwe wasemaji wa uchaguzi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewataka waangalizi wote wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu waliopata vibali, kutambua kuwa wao siyo watendaji bali wana jukumu la kutazama uchaguzi utakavyokuwa.

Mjumbe wa tume hiyo, Asina Omary, alitoa kauli hiyo alipofungua mafunzo kwa watazamaji wa ndani wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu kutoka Kituo cha Kimataifa cha Sera barani Afrika (CIP) jijini Dar es Salaam jana.

Asina alisema watazamaji hao wanapaswa kukumbuka kuwa wao siyo watendaji wa uchaguzi bali wajibu wao ni kutazama tu namna ambavyo shughuli nzima zinavyoendeshwa, ili kupata fursa ya kuandaa ripoti katika taasisi zao na kutoa mapendekezo mbalimbali.

"Kutazama uchaguzi ni jambo ambalo lipo kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, hivyo leo (jana) tumeamua kuwakumbusha majukumu ya kazi ili mwisho wa siku wahakikishe wanatazama vizuri uchaguzi huu ambao ni muhimu kwa Watanzania katika kupata viongozi bora watakaowaletea maendeleo," alisema.

Asina alisema NEC mpaka sasa imeshatoa vibali kwa taasisi na asasi 97 za ndani na 17 za nje kwa ajili ya kutazama  uchaguzi huo.

"Tunaendelea kutoa vibali vya taasisi mbalimbali zinazotaka kutazama uchaguzi kwani kwa mujibu wa sheria, watazamaji wanaruhusiwa kuwapo na kwenda kwenye kampeni za vyama mbalimbali vya siasa, kujitambulisha kwa wasimamizi wa uchaguzi, kuingia katika chumba cha kupigia kura kuangalia uchaguzi, kuhesabu kura pamoja na majumuisho ya kura hizo.

"Niwakumbushe tu watazamaji wa ndani wana fursa nyingi za kuangalia kwa uzuri na umakini uchaguzi huu kwa sababu wanaijua nchi yao na lugha kwa ufasaha kuliko wale wanaotoka nje ya nchi," alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya CIP, Profesa Rwekaza Mukandara, alisema wanaishukuru NEC na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kutoa vibali vya watazamaji wa kituo hicho ambao kazi yao itakuwa kuangalia mwenendo mzima wa uchaguzi nchini.

Alisema wanatoa mafunzo kwa watazamaji hao ili kuhakikisha wanakwenda kuifanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria, wawe waadilifu na makini pasipo kuegemea upande wowote.

"Tunataka watazamaji wetu wahakikishe kwamba wanachokiona ndicho watakachokitolea taarifa ili hatimaye tuweze kutoa ripoti ambayo ni sahihi na itakayoonyesha kwa ukamilifu yale yaliyojiri, yatatufanya  tuweze kuamua kama uchaguzi huu ulikuwa huru na haki," alisema Profesa Mukandara.

Mkurugenzi wa Programu kutoka CIP, Raymond Maro, alisema kituo hicho kimeingia kwa mara ya kwanza kutazama uchaguzi mkuu na kuchukua watazamaji 93 ambao watapelekwa Zanzibar na katika mikoa 17 ya Tanzania Bara.

Alisema baada ya mafunzo hayo, watazamaji hao watakwenda kukaa katika mikoa hiyo na wengine Zanzibar kwa takribani siku 10 kwa lengo la kutazama uchaguzi kulingana na sheria inavyotaka.

Habari Kubwa