NEC yaanika asasi elimu ya mpigakura

09Jul 2020
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
NEC yaanika asasi elimu ya mpigakura

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza asasi 245 za kiraia zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huku asasi 97 zimepewa kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi, huku saba zikiruhusiwa kutoa elimu ya mpigakura Visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Wilson Charles, PICHA MTANDAO

Kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye tovuti ya NEC juzi na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Wilson Charles, asasi hizo ziliwasilisha maombi Januari 20, mwaka huu.

“Baada ya uhakiki na kufanya upembuzi wa maombi yaliyopokelewa, taasisi/asasi saba zilikidhi vigezo na kustahili kupewa vibali kwa ajili ya kutoa elimu ya mpigakura kwa upande wa Tanzania Zanzibar,” alisema.

Alizitaja asasi hizo kuwa ni Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Pemba Association for Society Organization, Shirikisho la Michezo ya Viziwi Zanzibar.

Zingine ni Tanzania Women Political Enhancement Network Zanzibar Zone (TWOPENZZ), Umoja wa Madereva na Utingo Zanzibar (UMUZA), Umoja wa Ujirani Mwema Zanzibar (UJIMWEZA) na Zanzibar Fighting Against Youth Challenges Org.

“Tume inazitaka asasi zote zilizopewa vibali kuzingatia taratibu na kanuni zinazoongoza suala hilo, ikiwamo mwongozo wa utoaji wa elimu ya mpigakura…Asasi zilizopewa vibali zitalazimika kushiriki semina maalum ya kupitia mwongozo huo,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, mwishoni wa mwezi uliopita, Tume ilibainisha kasoro katika asasi zilizoomba vibali ikiwamo kutosajiliwa kwenye masjala, kutokuwa na ofisi, kushindwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo, kuwasilisha maombi ya kutoa elimu ya uraia badala ya elimu ya mpigakura.

Kasoro zingine ni kuwasilisha maombi bila kueleza maeneo zinayotaka kutoa elimu, malengo ya asasi kutoendana na utoaji elimu, kutowasilisha nyaraka muhimu kama katiba, cheti cha usajili na ratiba, kutowasilisha ordha kamili ya majina ya watendaji wakuu na kutoonyesha njia za mawasiliano.

Habari Kubwa