NEC yahamishia Dodoma shughuli za uchaguzi mkuu

15Jul 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
NEC yahamishia Dodoma shughuli za uchaguzi mkuu

SHUGHULI za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, ikiwamo utoaji fomu za ugombea urais zitafanyika jijini Dodoma baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuhamia rasmi katika ofisi zake mpya zilizopo Njedengwa.

Tangu kuanzishwa kwa Tume hiyo ilikuwa ikifanya shughuli hizo katika ofisi tatu tofauti jijini Dar es Salaam ambazo ni jengo la Posta, ofisi ndogo ya Mtaa wa Garden na Bohari ambako hutumika kama ghala la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi.

Akizungumza na kundi la kwanza la watumishi walioripoti katika ofisi hizo jijini hapa, Mkurugenzi wa Tume hiyo, Dk. Wilson Mahera, alisema hatua ya Tume kupata ofisi yake itaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuokoa fedha na muda uliokuwa unatumika kutoka ofisi moja hadi nyingine.

Alisema shughuli za uchaguzi mkuu wa Oktoba ikiwa ni pamoja na utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa urais katika uchaguzi huo sasa rasmi zitafanyika katika jengo hilo jipya lililopewa jina la Uchaguzi House.

Dk. Mahera aliwapongeza watumishi waliojitolea kutangulia Dodoma kwa ajili ya kuanza kazi katika ofisi hizo, huku akiwataka kujituma zaidi ili kazi zao ziakisi mwonekano wa ofisi hiyo.

Habari Kubwa