NEC yaikana orodha wabunge CHADEMA

12Nov 2020
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
NEC yaikana orodha wabunge CHADEMA

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haijapokea orodha ya majina ya wabunge wa viti maalumu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera, alisema tume bado haijapokea orodha hiyo kama ambavyo imekuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Kuna orodha ya majina inayosambaa kwenye mitandao ikionyesha majina ya wabunge wa Viti Maalumu wa CHADEMA. Orodha hiyo si ya kweli kwani hadi sasa hatujapokea orodha ya majina ya walioteuliwa kwenye nafasi ya ubunge wa viti maalumu kutoka chama hicho,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema amesikitishwa na taarifa ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, iliyodai kuwa orodha ya majina hayo ni ya tume.

“Tume tumesikitishwa sana kusikia Katibu wa CHADEMA, John Mnyika, akidai kuwa orodha ya majina ya wa bunge wa viti maalumu ni ya tume. Imetusikitisha sana kwa kuwa siyo kweli,” aliongeza.

Dk. Mahera alisema aliwasiliana na Mnyika kwa kumpigia simu na kumwandikia barua ya kuulizia orodha ya majina hayo na kumwambia asubiri mpaka atakapoyaleta yeye mwenyewe baada ya utaratibu wa chama kukamilika.

“Mnyika mwenyewe anafahamu kuwa bado hatujapokea majina na alisema atayaleta majina hayo yeye mwenye endapo watakamilisha utaratibu wao, hivyo mpaka sasa hivi, NEC hatujapokea majina kutoka CHADEMA ambayo yamesainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho,” alisema Mahera.

“Bado tunasubiri majina hayo ambayo yametiwa saini na kupigwa muhuri wa Katibu Mkuu wa chama kwa kuwa utaratibu ndio unaelekeza hivyo,” alisisitiza.

Kutokana na kuvuja kwa orodha hiyo, kuna taarifa kwamba Mnyika  alimwandikia barua Dk. Mahera, kutaka kupewa ufafanuzi kama tume imeshatangaza na kuwasilisha bungeni majina 19 ya wabunge wa viti maalumu wa chama hicho.

Aidha, tangu kutoka kwa mijana hayo kwenye mitandao, kumekuwa na taharuki juu ya chanzo halisi cha majini hayo, huku wapinzani, wakiwamo CHADEMA, wakiirushia lawama NEC kuwa ndiyo imehusika.

Habari Kubwa