NEC yakamilisha uandikishaji mikoa 25

11Jan 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
NEC yakamilisha uandikishaji mikoa 25

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekamilisha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura katika mikoa 25 yenye halmashauri za wilaya 146 na majimbo 205 Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa NEC, mikoa ya Tanzania Bara amabyo kazi hiyo imefanyika ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara, Mwanza, Kigoma, Tabora, Songwe, Kagera, Geita, Shinyanga, Katavi, Rukwa na Singida.

Mingine ni Dodoma, Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma huku Zanzibar ikiboresha katika mikoa ya mikoa ya Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Mjini Magharibi.

Kwa mujibu wa taarifa ya NEC kwa vyombo vya habari jana, tume kwa sasa inajiandaa kuanza uboreshaji wa daftari katika mikoa ya Lindi na Mtwara na kwamba tayari mikutano ya wadau wakuu wa uchaguzi imefanyika.

Katika taarifa hiyo, NEC pia ilieleza kuwa elimu na hamasa kwa wananchi inaendelea kutolewa katika mikoa hiyo na kazi hiyo inatarajiwa kufanyika kwa siku saba kuanzia Januari 12 hadi 17.

NEC ilieleza katika taarifa yake hiyo kuwa awamu zilizobaki katika ukamilishaji wa kazi ya uboreshaji wa daftari hilo zinajumuisha mikoa ya Tanga na Morogoro katika Halmashauri za Miji ya Ifakara, Wilaya ya Malinyi na kazi itafanyika kuanzia Januari 23 hadi 29.

Tume hiyo ilisema itaendelea na uboreshaji wa daftari hilo katika wilaya za Gairo, KIlombero, Kilosa, Morogoro na Mvomero hadi Februari 9 mwaka huu.

Kwa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, uboreshaji umepangwa kufanyika kuanzia Februari 10 hadi 16.

NEC ilisema mchakato wa uboreshaji wa daftari hilo utahitimishwa kwa uwekaji wa wazi daftari hilo ili kutoa fursa kwa wananchi kuhakiki taarifa zao.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ina jukumu la kuandikisha wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

“Hivi sasa tume iko katika utekelezaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Uboreshaji huu unawahusu raia wa Tanzania ambao wametimiza miaka 18 na wale ambao watatimiza umri huo siku ya uchaguzi Oktoba.”

“Pia unawahusu wale ambao wamehama kutoka maeneo yao ya awali kwenda maeneo mengine ya uchaguzi na wale ambao kadi zao zimeharibika au kupotea pamoja na kuwaondoa wale ambao wamepoteza sifa ya kuwapo katika daftari hilo hususani waliofariki dunia," NEC ilifafanua zaidi katika taarifa yake hiyo.

Habari Kubwa