NEC yakunjua makucha wagombea kuhusu matusi

30Sep 2020
WAANDISHI WETU
Dodoma
Nipashe
NEC yakunjua makucha wagombea kuhusu matusi

ZIKIWA zimesalia siku 29 kufanyika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewataka wagombea na vyama vya siasa kuzingatia maadili ya uchaguzi kwenye kampeni na kuepuka lugha za uchochezi zinazotishia usalama wa nchi.

Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salim Mbarouk.

Aidha, imewahakikishia Watanzania kuwa itasimamia uchaguzi huo kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na taratibu ili uwe huru na haki.

Akifungua jana mkutano wa tume hiyo na wadau wa uchaguzi mkoani hapa, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salim Mbarouk, alisema wagombea kwenye kampeni zao wanapaswa kujiepusha na lugha za kashfa.

Jaji Mbarouk alisema kunapokuwa na malalamiko yoyote ya kimaadili, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kuwasilisha malalamiko kwenye Kamati za Maadili ndani ya muda uliowekwa.

“Tunawakumbusha kipindi hiki sheria nyingine za nchi hazijasimama, hivyo wajihadhari na vitendo au matamshi ambayo yatasababisha vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi,” alisema.

Aliwahakikishia wadau kuwa tume hiyo itahakikisha uchaguzi mwaka huu unakuwa huru, wazi, haki na wa kuaminika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea.

“Pia tunawatoa hofu wapigakura wenye mahitaji maalum kwa kuwa tumeshatoa maelekezo kwa watendaji kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu, wajawazito, akina mama wanaonyonyesha waliokwenda na watoto vituoni, wazee na wagonjwa,” alisema.

Kadhalika, alisema kwa wasioona kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na kifaa cha maandishi ya nukta nundu.

Akizungumzia kuhusu vifaa, makamu mwenyekiti huyo alisema NEC inaendelea na mchakato wa ununuzi wa vifaa na uchapishaji wa nyaraka na kwamba zabuni zote zimeshatangazwa na zinahusisha uchapishaji wa fomu mbalimbali.

 Jaji huyo alisema tume inatarajia kuwa na vituo vya kupigia kura 80, 155 kati ya hivyo 79,670 vya Tanzania Bara na 485 Zanzibar na pia itatumia vituo 1,412 vya ZEC kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

“Kila kituo kati ya hivyo, kitakuwa na wapiga kura wasiozidi 500. Orodha ya vituo imewasilishwa kwa wasimamizi wa uchaguzi kwa ajili ya maandalizi na viongozi wa vyama vya siasa ngazi ya jimbo watapatiwa hiyo orodha siku 14 kabla ya siku ya uchaguzi ili kuwawezesha kuwasilisha orodha ya majina ya mawakala watakaopangwa kwenye vituo,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpigakura, Giveness Aswile, alisema vifaa vingine vimeanza kupokelewa na karatasi za kura zitakuwa za mwisho kutolewa kutokana na mchakato wake kuwa mrefu.

Aidha, alisema kwenye vituo hivyo kutakuwa na watendaji 320,620 ambao watasimamia na kuendesha upigaji kura vituoni.

Habari Kubwa