NEC yaonya wasimamizi kuzima simu

04Aug 2020
Na Waandishi Wetu
Tabora
Nipashe
NEC yaonya wasimamizi kuzima simu

WASIMAMIZI wa uchaguzi wa mikoa na wasimamizi wa uchaguzi mkuu ngazi ya wilaya na majimbo, wameagizwa kuhakikisha simu zao zinakuwa wazi katika kipindi chote hadi uchaguzi utakapomalizika na matokeo kutangazwa rasmi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kadhalika, NEC imewasisitiza wasimamizi wa uchaguzi mkuu ngazi ya majimbo kutoka Shinyanga na Simiyu, wakasimamie vizuri uchaguzi huo ili ufanyike huru na haki, bila ya kusababisha dosari zozote zile ambazo zitaleta vurugu na kuchafua amani ya nchi.

Marufuku ya wasimamizi kutozima simu ilitolewa jana mjini Tabora na Ofisa wa NEC, Edward Makono, wakati wa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi 110 kutoka mikoa na Kigoma na Tabora.

Alisema lengo la kuwataka simu zao kuwa wazi ni kuhakikisha kuwa wanakuwa tayari kila wakati kupata maelekezo yanayohusu masuala ya uchaguzi na upokeaji wa vifaa vya uchaguzi vitakapoanza kugawiwa katika maeneo mbalimbali wanayosimamia.

“Mkiwa wasimamizi wa uchaguzi wanatakiwa kuwa tayari wakati wote hata ikibidi kupunguza baadhi ya shughuli binafsi ambazo zinaweza kuathiri uchaguzi…mnapolala lala ukiwa tayari na wala usizime simu yako wakati wote,” alisisitiza.

Alisema kitendo cha kuzima simu kinaweza kusababisha msambazaji wa vifaa vya uchaguzi kuchelewa kufika katika vituo vinavyofuata, hivyo kuchelewesha uchaguzi.

Makono alisema msimamizi yeyote ambaye atasababisha vifaa vichelewe kupokelewa kutokana na simu yake kutopatikana, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa umma na za NEC.

WAONYWA KUVURUGA AMANI

Katika hatua nyingine, NEC imewasisitiza wasimamizi wa uchaguzi mkuu ngazi ya majimbo kutoka Shinyanga na Simiyu, wasimamie vizuri ili ufanyike katika mazingira huru na haki, bila ya kusababisha dosari zozote zile ambazo zitaleta vurugu na kuchafua amani ya nchi.

Hayo yalibainishwa jana mjini Shinyanga na Kamishna wa NEC, Omari Ramadhan Mapuri, wakati akifunga mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi mkuu wa mikoa ya Shinyanga na Simiyu.

Alisema hatima ya amani ya nchi kwenye uchaguzi mkuu ipo mikononi mwa wasimamizi, ambao wanapaswa kuzingatia sheria za uchaguzi pamoja na maelekezo ya tume ambayo wamepewa kwenye mafunzo, ili kufanikisha uchaguzi huo ufanyike kwa haki.

“Naombeni sana wasimamizi wa uchaguzi mkuu mzingatie mafunzo ambayo imepewa na tume, pamoja na kufuata sheria za uchaguzi, na kutofanya kazi kimazoea ili uchaguzi ufanyike kwa uhuru na haki,’ alisema Mapuri.

“Kwenye changamoto kubwa ambazo hamna uwezo wa kuzitatua wasilianeni na tume zitatuliwe, ili kuepuka kujiingiza kwenye migogoro.”

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpigakura wa NEC, Givness Aswile, aliwataka wasimamizi hao mafunzo ambayo wamepewa wayatoe pia kwa ufasaha kwa wasimamizi ngazi ya kata, ili uchaguzi ufanikiwe ngazi zote na kumalizika salama.

Imeandikwa na Tiganya Vincent, TABORA na Marco Maduhu, SHINYANGA

Habari Kubwa