NEC yapongezwa elimu mpigakura

22Oct 2020
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
NEC yapongezwa elimu mpigakura

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepongezwa kwa kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya mpigakura katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya The Right Way (TRW), Wallace Mayunga, alisema NEC imejitahidi kutoa elimu,  itakayosaidia kuondoa malalamiko na uchaguzi kuwa wa huru.

Mayunga alisema, bado makundi mbalimbali yanapaswa kuendelea kufikiwa ili kupata elimu hiyo yakiwamo makundi ya wafugaji, wakusanya matunda pamoja na vijana.

“Tumeshuhudia kampeni za sasa zimekuwa za kistaarabu pamoja na kuwa kuna baadhi ya viashiria visivyo vizuri, lakini vyombo vya dola vimekabiliana navyo kwa amani,” alisema.

Mayunga aliwaomba waandishi wa habari kuhakikisha wanasaidiana na serikali kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kushiriki uchaguzi usiotokana na rushwa.

Alisema rushwa ya uchaguzi ni tishio kwa chaguzi huru na haki, kwa kuwa rushwa ya aina hiyo inaleta viongozi wasio sahihi na kusababisha kuwapo kwa serikali ya kifisadi.

Mayunga alisema jitihada mbalimbali zinafanywa na serikali kuhakikisha taasisi za umma na vyombo vya dola havitumiki kuchochea matokeo ya uchaguzi.

“Hata chama tawala kimetengwa kabisa na serikali na kwamba hakitumii vibaya nafasi yake kisiasa na vyama vyote vya siasa vinapewa fursa sawa," alisema Mayunga.

Aliwashauri watu wote wenye sifa ya kupiga kura kujitokeza kupiga kura bila kizuizi.

“Vyama vya siasa, wagombea na asasi za kiraia zinapata fursa ya kuufikia umma kwa lengo la kutoa elimu ya uraia bila kuwapo kwa kizuizi cha aina yoyote,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRW, Justina Shauri, alisema kuwa wao watazamaji wa uchaguzi watahakikisha wanatoa taarifa ya kile walichokiona katika maeneo mbalimbali na si vinginevyo.

Shauri alisema, kuwa wameweka watazamaji katika mikoa 11 nchini ambao wataangalia mwenendo wa uchaguzi na kisha kutoa ripoti ya namna uchaguzi huo ulivyofanyika.

“Sisi tunafuata maelekezo tuliyopewa na NEC hatuwezi kutoka nje ya hiyo, hivyo tutaangalia vyote vinavyojitokeza katika maeneo ya uchaguzi na kisha tutatoa ripoti yetu,” alisema.

Aliwataka waangalizi hao kuhakikisha hawapendelei chama kimoja na wasikwende kinyume na majukumu yao.

Habari Kubwa