NEC yataja vigingi vinne uchaguzi mkuu

21Nov 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
NEC yataja vigingi vinne uchaguzi mkuu

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetaja kero nne ilizokutana nazo wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu, ikiwamo baadhi ya wagombea kuwatisha wasimamizi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Charles, picha mtandao

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Charles, aliyasema hayo jana wakati wa kikao cha tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kilichohudhuriwa na waratibu wa uchaguzi wa mikoa na wasimamizi wa majimbo yote nchini.

Alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana kulikuwa na kero chache, kwamba katika uchaguzi huo kulikuwa na vitisho vya simu kwa wasimamizi kuanzia ngazi ya majimbo hadi  taifa.

“Tunashukuru Mungu jambo limeisha maana kulikuwa na vitisho na matusi ambavyo vilikuwa vikitolewa na baadhi ya viongozi wa vyama kwa wasimamizi na Mkurugenzi wa Uchaguzi kwa njia ya simu,” alisema Dk.Charles.

Alitaja kero nyingine kuwa ni kutozingatiwa kwa ratiba za kampeni za uchaguzi na kuingilia ratiba za wagombea wengine.

“Kulikuwa na mwingiliano wa ratiba, baadhi ya vyama vilikuwa vikiingilia ratiba za vyama vingine katika mikutano ya kampeni za uchaguzi na kugoma kushuka jukwaani,”alisema Dk.Charles.

Alisema kulikuwapo na wagombea ambao walikuwa wanapitisha muda uliopangwa wa kunadi sera zao pindi walipokuwa jukwaani.

“Kulikuwa na tatizo la wagombea kupitisha muda wa saa 12 jioni uliopangwa wa kufanya kampeni, mtu anakataa waziwazi anaambiwa shuka anasema sishuki, lakini nawapongeza askari kwa kuchukua hatua sasa hayo yamepita,”alisema Dk. Charles.

Alitaja kero nyingine ni baadhi ya vyama vya siasa wagombea wake kutokutii maagizo ya Kamati ya Maadili.

“Baadhi ya vyama vya siasa kutotii wito wa Kamati ya Maadili na ukiukwaji wa maadili wakati wa mchakato mzima wa kampeni, hili nalo lilijitokeza,”alisema Dk. Charles.

Kadhalika, alitaja kero ya nne kuwa ni idadi kubwa ya rufaa walizozipokea ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2015.

“Kulikuwa na mapingamizi ya kutosha sijui ni kwa sababu ipi? Lakini mengi yalikuwa ya wagombea kwa wagombea. Hii ilituletea shida kupitia na rufani zilikuwa nyingi,” alisema Dk. Charles.

Aidha, alisema idadi ya wapigakura katika uchaguzi huo ilikuwa ni asilimia 51 ambapo idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2015 iliyokuwa asilimia 49.

Aidha, alibainisha kuwa asilimia 17 ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani ambao wameshindwa kurudishwa baada ya kukata rufaa ni kutokana na kukosa sifa na kama wataenda mahakamani hawatashinda.

Dk. Charles alisema asilimia 83 ya rufaa zilizokatwa waliwarejesha kwenye uchaguzi, huku asilimia 17 hawakurudishwa.

“Niwapongeze kwa kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwa sababu mlikuwa wepesi kukusanya matokeo, lakini mlikusanya kwa wakati na tulishirikiana vizuri na watu wa Tehama, hakika zile sifa za kutangaza matokeo ndani ya saa 48 tunazirejesha kwenu yote haya kwa sababu tulikuwa tunafanya kwa pamoja,”alisema Dk. Charles.

Kuhusu madiwani vitimaalumu, Mkurugenzi huyo alisema walikaa kikao kupitisha vyama ambavyo tayari vimeshawasilisha majina.

“Watu wanadhani majina tunapitisha sisi, sisi tunapokea orodha kutoka kwenye vyama, halafu sisi tunateua, mara nyingi watu wamekuwa wakisumbua kwamba sisi ndiyo tunapanga siyo kweli,”alisema Dk. Charles.

Habari Kubwa