NEC yatakiwa kuwajengea mazingira makundi maalum

06Jul 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
NEC yatakiwa kuwajengea mazingira makundi maalum

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetakiwa kuweka mazingira mazuri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupiga kura kwa usalama katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa jana na wadau wa haki za binadamu katika kikao mkakati juu ya ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika nafasi za uamuzi na uongozi kilichowakutanisha wadau mbalimbali vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mahakama.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mathew Mwaimu, alisema Tume hiyo ina wajibu wa kuwafanya wananchi kushiriki katika uchaguzi vizuri zaidi kama haki yao ya msingi kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni.

Alisema NEC ihakikishe inawaandaa wananchi kushiriki uchaguzi katika mazingira ya amani na kuzingatia misingi ya afya hasa katika kipindi cha ugonjwa wa corona.

Mkurugenzi wa Kituo cha Amani, Haki na Msaada wa Kisheria (PLAJC), Jaruo Karebe, alisema kikao hicho kimelenga kuweka mazingira wezeshi na kuimarisha ushiriki wa watu hao katika mchakato wa uchaguzi na kuendeleza uhusiano imara wa kikazi kati ya asasi za kiraia, taasisi za serikali na vyama vya siasa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi.

Naye Ofisa kutoka TAKUKURU, Tulibako Minga, aliwaonya wananchi kutojihusisha na masuala ya rushwa kwenye uchaguzi mkuu kwa kuwa hawataangalia jinsia ya mtu bali watawakamata kwa mujibu wa sheria.

Habari Kubwa