NEC yatangaza uchaguzi kumrithi Lissu 

06Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
NEC yatangaza uchaguzi kumrithi Lissu 

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Singida Mashariki, mkoani Singida utakaofanyika Julai 31, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),  Jaji Semistocles Kaijage

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),  Jaji Semistocles Kaijage,  alitangaza hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam na kusema kuwa ratiba inatokana na barua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, inayoeleza kuwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu (Chadema), amepoteza sifa ya kuwa mbunge.

Katika taarifa ya Spika Ndugai, alitaja sababu za Lissu kuvuliwa ubunge kuwa ni kushindwa kuwasilisha tamko la mali na madeni na kutohudhuria mikutano saba mfululizo bila ruhusa ya Spika.

"Tumezingatia  matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, kutoa taarifa kwa umma kuhusu uwapo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki," alisema Jaji Kaijage.

Jaji Kaijage alisema fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya Julai 13 na 18 mwaka huu, na uteuzi wa wagombea utafanyika Julai  18.

Alisema kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30 na siku ya uchaguzi itakuwa Julai 31, mwaka huu.

Aidha, alivikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na tume hiyo wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo.

Wiki iliyopita, Spika Ndugai katika taarifa yake ya kuahirisha mkutano wa Bunge la Bajeti mjini Dodoma, alitangaza kumvua ubunge Lissu wakati akiwa ameshawasilisha taarifa hiyo kwa NEC kwa ajili ya kuitisha uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Ndugai alisema kanuni za bunge na katiba ya nchi zinataka mbunge huyo avuliwe ubunge kwa kutotimiza masharti ya kuendeleza ushiriki wake katika shughuli za bunge.

Lissu ambaye alikuwa mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni kuanzia 2015 alikwenda nje ya nchi tangu aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiyojulikana akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba, 2017.

Baada ya kunusurika katika shambulizi hilo Lissu alisafirishwa hadi Nairobi, Kenya kwa matitabu ya dharura na baadaye nchini Ubelgiji ambako amekuwa akipata matibabu kwa miezi kadha sasa.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Lissu akiwa ameanza kupata nafuu kubwa alitembelea nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Uingereza, Marekani na kuilaumu serikali kwa kushindwa kupata ufumbuzi kuhusu shambulizi dhidi yake.

Mwanasiasa huyo pia alitangaza mwezi uliopita kuwa anapanga kurejea nchini Septemba mwaka huu ikiwa ni miaka miwili tangu kunusurika shambulizi la kutaka kumuua.

Habari Kubwa