NECTA kuanza kusahihisha mitihani kidijitali mwezi huu

02May 2022
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
NECTA kuanza kusahihisha mitihani kidijitali mwezi huu

MFUMO mpya wa usahihishaji mitihani kidijitali unaosimamiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kwa watahiniwa wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu unatarajiwa kuanza kazi kwa mara ya kwanza mwaka huu, ukianza na mitihani ya walimu, inayofanyika wiki ijayo.

Ofisa Uhusiano wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), John Nchimbi akizungumza na mwandishi wetu. PICHA: NIPASHE DIGITAL

Matumizi ya teknolojia ya kielektroniki kusahihisha yataokoa fedha, muda na kuongeza ufanisi, Ofisa Habari na Uhusiano NECTA, John Nchimbi, anasema katika mahojiano maalum na Nipashe.

Majaribio ya matumizi ya mfumo huo yamekwishafanyika kwenye vyuo vyote vya ualimu nchini, kujiandaa na usahihishaji kidijitali ambao unaanzia mitihani ya watahiniwa wa ngazi ya cheti na diploma ya ualimu, inayotarajia kuanza wiki Ijayo Mei 9, 2022.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika Dar es Salaam, Nchimbi anasema NECTA imepanga kuwa ifikapo 2025 usahihishaji kidijitali utafanywa kwa mitihani yote ikiwamo ya darasa la nne na ya kumaliza elimu ya msingi, kidato cha pili, cha nne, sita na ya ualimu.

Endelea na Mahojiano…..

SWALI: Unaweza kutufafanulia zaidi kuhusu mfumo wa usahihishaji mitihani uliozinduliwa hivi karibuni na NECTA?
JIBU: Ili kuufahamu mfumo mpya wa kidigitali, nizungumzie wa kianalojia uliotumika kwa miongo mingi.

Baraza tunavyosahihisha mitihani kwa sasa tunawatumia watahini au wasahihishaji kutoka sehemu mbalimbali nchi nzima.

Mfano, mtihani wa kidato cha nne tunaweza kuwa na vituo kama nane vya kazi, mtihani wa hisabati unaweza ukasahihishwa Dar es Salaam, Fizikia Kigoma, Kemia Morogoro na sehemu nyingine mbalimbali.

Hawa watahini wakiitwa kwenye kituo cha usahihishaji wanakaa kwenye jopo mtihani mmoja, jopo linaweza kuwa na maswali saba, nane hata   10, kila msahihishaji anapewa swali lake.

Tunaita mnyororo wa usahihishaji unaozunguka kutoka swali la kwanza hadi la mwisho kila mmoja kwa swali lake. Mtihani ukishasahihishwa unakwenda kwa mhakiki kuhakikisha usawa wa kile kilichosahihishwa, akiona kimekaa sawa ataupeleka kwa mtu anayeingiza alama kwenye kompyuta.

Hatua nyingine hufuata, kwa kifupi usahihishaji mtihani wa kitaifa unazingatia vitu vingi kwa wanajopo. Mfumo huu wa analojia unatumiwa na nchi mbalimbali na wengine walikuja kujifunza kwetu.

Tofauti na mitihani ya kawaida mwalimu wa somo fulani atasahihisha somo hilo hilo maswali yote, hii inamchosha na pia ufanisi unapungua.

Sasa tunaingia kwenye kusahihisha kidijitali au kielektroniki 'electronic marking' na mwaka huu unaanzia mitihani ya ualimu. Mfumo hautowalazimu watahini kukutana kwenye kituo cha usahihishaji.

Badala ya kukusanya watu, watakaa pale walipo wanapofanyia kazi ila wanapaswa wawe na kompyuta.

Msahihishaji atapewa nywila au neno la siri (password) na NECTA , atasubiri muda ukifika akifungua kompyuta mfumo utakuja. Badala ya kuwa na karatasi za mitahani, kalamu nyekundu kama zamani, sasa atatumia 'mouse' au kipanya.

Mfumo unabainisha jibu hili lina alama kadhaa kulingana na mwongozo wa usahihishaji.

SWALI: Kabla ya kusahihisha maswali msahihishaji anayaona kwenye kompyuta? Mfano, mtihani una maswali 20, naye anatakiwa kusahihisha swali moja, Je, atayaona yote au lile linalomhusu?

JIBU: Mtu anayesahihisha anaona swali lake tu. Akisha ‘save’ swali linaondoka, linakuja la mwanafunzi au mtahiniwa mwingine ila ni lilelile moja linalomhusu.

SWALI: Mitihani ipi itahusika?

JIBU: NECTA tunahusika na mtihani wa darasa la nne, la saba, kidato cha nne, sita, walimu ngazi ya cheti na diploma. Usahihishaji wa kidijitali kwa mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, mwaka 2012 wanafunzi wakianza kufanya mtihani kwa kutumia karatasi za OMR (Optical Mark Reader), mtihani ulijibiwa kwa maswali ya kuchagua, mashine iliskani mtihani uliojibiwa na kusahihisha.

Mfumo ukabadilika baadaye maswali badala ya kuwa ya kuchagua yote, ikawa 40 ya kuchagua na matano ya kujibu kwa kuandika au kufanya mahesabu. Hivyo 40 yalisahihishwa kwa ‘scanner’ na haya matano ilimlazimu msahihishaji atumie kalamu.

Ila mwaka jana tukasema hapana, haya maswali yote yaingizwe katika mfumo wa kidijitali. Mwaka huu mitihani ya walimu itasahihishiwa kidijitali.

Mwakani tunatarajia kidato cha sita usahihishwe kidijitali na 2024 utakuwa wa kidato cha pili na 2025 utakuwa wa sekondari.

SWALI: Matumizi ya teknolojia yatarahisisha kazi na kupunguza muda wa kazi, ingawa mijadala kwenye jamii ni kuhusu maswali ya kujieleza hujibiwa kwa uelewa tofauti, inakuwaje kwenye kutoa alama?

JIBU : Ili mtu aelewe usahihishaji kidijitali ni lazima auelewe huu wa analojia ambao tumeutumia hapo awali. Jamii ijue kabla usahishaji haujaanza huwapo majadiliano, kwamba swali la kwanza lina alama tano, mtu akipewa swali la kujieleza atatumia mwongozo na uzoefu wa kazi ya usahihishaji kulingana na anavyoliona kwenye kompyuta.

Mtahini au msahihishaji atasahihisha kulingana na mwongozo. Kilichobadilika ni kwamba mfumo huu hautumii kalamu, hauwakusanyi wasahihishaji ila mtu atatumia kompyuta na kuliona swali na jibu la mtahiniwa na kutoa alama.

Watanzania waondoe hofu kuhusu usahishaji kidijitali.

SWALI: Baada ya majibu kutunzwa kwenye kompyuta au kidijitali hakuna changamoto au hatari ya kufanyiwa udukuzi kwenye mfumo na kupoteza ya mitihani ya nchi nzima?

SWALI: Mifumo hii imeundwa na wataalamu IT wa NECTA, unaweza ukaingiliwa lakini ni rahisi kupata (recover), tumeweka vidhibiti, ili iwe rahisi kwa wataalamu wetu kudhibiti.

SWALI:Vipi kuhusu kompyuta za usahihishaji ni za kutosha?

JIBU: Sehemu ziliko na vituo vya usahihishaji kuna kompyuta na pia baraza tumejipanga. Tutaifanya kazi hii kwa ifanisi.
 
Aprili 20, mwaka huu vyuo vyote vya ualimu yamefanyika majaribio ili kujiridhisha iwapo mfumo huu utafanikiwa.
Mfano tu, kuanzia mwaka 2020 tulianza kutumia karatasi za OMR, ambazo ni maalum kwa kufanyiwa 'scanning' katika kompyuta, zinazotengezwa ndani ya nchi, wakati wa corona ulitufunza kujiongeza na kufikiri  kujitegemea.  

SWALI: Ni yepi manufaa ya mfumo huu, kiuchumi?

JIBU: Nitoe mfano tu mtihani wa kidato cha nne, cha pili na darasa la nne mwaka jana kazi ya kusafirisha watahini au wasahihishaji 28,000 tulitumia milioni 500 ambao walitoka maeneo yao hadi kituo cha usahishaji, chakula kiligharimu bilioni tisa hapo hujaweka posho.

Mwaka huu ambao watasahihisha mitihani ya walimu tutaokoa Sh. milioni 550. Kuna ongezeko la watahiniwa baada ya sera ya elimu bure.

Kwa hiyo mfumo huu utarahisisha kazi. Tunahamasishwa kutumia TEHAMA kufanya kazi kwa ufanisi na kuokoa pesa ili kuongeza ufanisi na tija.

Kwa mfumo huu tutahakikisha mtahiniwa haki yake inapatikana, haya ni maisha.

Habari Kubwa