Dk. Msonde amesema udanganyifu huo umefanywa na wakuu wa shule 38 kwa kuhusisha wanafunzi wa sekondari waliomaliza masomo kuufanya mtihani huo na kuwapa wanafunzi.
Amesema katika shule ya Msingi Dominion iliyopo Arusha Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo alijificha chooni na wanafunzi walikuwa wakimfuata kwa awamu kuchukua majibu.
"Ofisa wa baraza aliyekuwa shuleni hapo baada ya kupata taarifa ya kuwa siku ya mitihani kutakuwa na udanganyifu, awali aliona wanafunzi wakitoka wanakwenda chooni lakini alishtuka baada ya kuwaona bila kujali jinsia wanaingia choo cha aina moja.
" Ndipo ofisa wetu alipofuatilia na kumkuta mwanaume akiwa amevaa mavazi ya wapishi akiwa amekaa chooni na majibu ya mtihani huu, alikamatwa na kufungiwa kwenye darasa moja lakini baada ya mtihani kuisha, walipofungua mlango ili kumkamata walikuta ametoroka kwa kupitia darini, ila alikamatwa baada ya msako kufanyika," amesema
Aidha Dk. Msonde amesema udanganyifu kama huo wamebaini unataka kufanyika katika mitihani ya kidato cha nne inayotarajia kufanyika Jumatatu ambapo mpaka sasa wamepata taarifa kwa shule 71 na kuzipa onyo.