Neema ajira 5,000 serikalini

25Apr 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Neema ajira 5,000 serikalini

SERIKALI imetangza kutoa ajira 5,410 kwa Jeshi la Polisi, Magereza, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

 

Akiwasilisha jana bungeni jijini Dodoma, hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alisema lengo kuwapo kwa ajira hizo ni kuimarisha usalama nchini.

Lugola alisema ajira hizo zitakwenda sambamba na kuwapandisha vyeo maofisa, wakaguzi na askari na kutoa mafunzo ya kitaaluma na kimedani ndani na nje ya nchi.

Alisema wizara yake itaimarisha upekuzi wa askari na vijana wanaoomba kujiunga kwenye majeshi hayo ili kuwa na askari wenye nidhamu na moyo wa kulitumikia taifa.

"Katika mwaka 2018/19, Jeshi la Polisi limeajiri askari wapya 812 kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kazi za polisi.

Askari hao wamehitimu mafunzo ya awali katika Shule ya Polisi (MPA), Aprili 9, mwaka huu," alisema.

Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2019/20, jumla ya askari 3,725 wanatarajiwa kuajiriwa kupitia Jeshi la Polisi huku akibainisha kuwa maofisa na askari 55 wanashiriki operesheni za ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali zikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia na Lesotho.

Alisema wizara hiyo inaomba kuidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 921. 247 kwa ajili ya bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha.

MAUAJI YA WATOTO NA VIKONGWEKuhusu mauaji ya watoto na vikongwe, waziri huyo alisema miezi ya Novemba na Desemba mwaka jana, yaliibuka matukio ya mauaji na utekaji watoto kwenye mikoa ya Njombe na Simiyu.

"Matukio hayo ni uhalifu mpya kutokea katika mikoa hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012. Katika mikoa ya Njombe, watoto sita waliuawa na watatu walitekwa ambapo polisi walifanikiwa kuwapata watoto waliotekwa wakiwa hai.

Kutokana na matukio hayo, watuhumiwa saba walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria," alisema.

Alisema KUWA katika Mkoa wa Simiyu kulitokea mauaji ya watoto wanne ambao waliuawa na kukatwa baadhi ya viungo. Alisema watuhumiwa 12 walikamatwa na kufikishwa mahakamani kutokana na matukio hayo.

Waziri huyo alisema polisi wamefanikiwa kudhibiti mauaji ya vikongwe kutoka 117 yaliyoripotiwa mwaka 2017/18 hadi matukio 57 kwa mwaka huu wa fedha.

"Hali inaonyesha mauaji ya vikongwe yamepungua kwa asilimia 51.3. Matukio hayo yalijitokeza kwenye mikoa ya Geita (7), Iringa (1), Kigoma (2), Lindi (1), Mbeya (3), Mwanza (6), Njombe (3), Rukwa (2), Ruvuma (2), Shinyanga (3), Simiyu (4), Songwe (7) na Tabora (16).

 

Habari Kubwa