NEMC: Elimu imedhibiti magonjwa ya mlipuko

22Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
NEMC: Elimu imedhibiti magonjwa ya mlipuko

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeeleza kuwa kupungua kwa kasi ya magonjwa ya mlipuko hususani kipindupindu nchini, kumetokana na usimamiaji mzuri wa sheria na kanuni za mazingira na utoaji wa elimu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, aliwapongeza Watanzania kwa kuweka mazingira safi na salama kwa hiari.

“Tabia ya kuchukia uchafu na kutunza mazingira ambayo imejengeka katika jamii yetu, ni jambo zuri sana. Kuheshimu sheria ya mazingira na kanuni zake kwa hiari ni kitu muhimu katika kulinda na kutunza mazingira, kulinda afya za watu na viumbe wengine,” alikiambia kikundi cha watu alichokikuta kinasafisha eneo lao kwa hiari.

“NEMC katika kipindi cha miaka mitano tumetoa elimu kupitia vyombo vya habari na kuandaa mikutano mbalimbali ya wadau wa mazingira na wananchi kwa ujumla wake.

Tumepata mafanikio makubwa kwani takwimu zinaonyesha magonjwa ya milipuko kama kipindupindu kasi ya kuenea kwake imepungua sana, sikumbuki kama tumekumbana na kipundupindu miaka mitano iliyopita,’’ alisema.

Aliongeza kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya milipuko nchini ni utiririshaji wa majitaka katika maeneo ya makazi ya watu pamoja na maji ya kemikali zenye sumu kutoka viwandani ambayo huelekezwa katika mito na makazi ya watu.

Habari Kubwa