New MV Victoria yaanza kutoa huduma leo

14Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
New MV Victoria yaanza kutoa huduma leo

KAIMU Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL) Abel Gwanafyo, amesema ukarabati na ukaguzi wa meli ya New MV Victoria uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 9 tayari umekamilika na inatarajia kuanza kutoa huduma ya usafiri leo oktoba 14, 2021.

Meli New MV Victoria ilisitisha kutoa huduma mnamo Septemba 22 mwaka huu ili kupisha ukarabati na ukaguzi wa kawaida unaofanyika kila baada ya mwaka mmoja.

Amesema meli hiyo itaanza safari zake leo kutokea jijini Mwanza kuelekea Bukoba mkoani Kagera, wakati Tanzania ikitimiza miaka 22 tangu kifo cha Baba wa Taifa Julius Nyerere.

"Ukarabati na ukaguzi uliyofanyika ni pamoja na ukaguzi wa wafanyakazi wa ndani ya meli, uwekaji na ukaguzi wa vifaa vya kuzima moto, kujaribu boti za dharura na maboya," amesema Gwanafyo.

Akizungumzia uboreshaji wa huduma katika meli hiyo Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma Abdullahman Salim, amesema ukarabati huo umeambatana na uboreshaji wa huduma za chakula na vinywaji ndani ya meli hiyo.

Amesema kampuni hiyo imeongeza aina za vyakula ndani ya meli hiyo huku bei yake ikiwa ni kuanzia shilingi 1,500 tofauti na awali ambapo bei ya chakula ilianzia 5,000.

Habari Kubwa