NGO 4,900 hatarini kufutiwa usajili

14May 2022
Na Mwandishi Wetu
IRINGA
Nipashe
NGO 4,900 hatarini kufutiwa usajili

ZAIDI ya mashirika 4,900 yasiyo ya kiserikali (NGO) yako hatarini kufutiwa usajili kutokana na kukiuka sheria na taratibu zinazoyaongoza.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju.

Kutokana na kukiuka huko, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, ameyataka kujieleza kwa nini yasifutiwe usajili kwa kitendo hicho.

 

Mpanju alitoa agizo hilo jana alipokutana na NGO za Mkoa wa Iringa katika ziara yake ya siku mbili mkoani hapa yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya wizara.

 

Mpanju alisema mashirika hayo yameshindwa kutekeleza matakwa ya kisheria ikiwamo kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya uhakiki, lakini tangu uhakiki huo uanze  mwaka jana, yameshindwa kufanya hivyo.

 

"Hadi kazi hiyo ya uhakiki inakamilika Machi, mwaka huu, ni mashirika 4864 kati ya 12,884 yamehakikiwa na mashirika 7,533 ndiyo yako hai. Sasa niwaombe NaCONGO

(Baraza na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali) hakikisheni yale mashirika ambayo hayakuhakikiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, yaeleze sababu kwa nini yasifutiwe ndani ya mwezi mmoja. Hapa  Iringa ni mashirika 79 kati ya 170," alisema.

 

Naibu Katibu Mkuu  alisema serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na mashirika hayo katika kutekeleza shughuli na huduma mbalimbali kama elimu, afya maji na huduma mtambuka ikiwamo kusaidia kupambana na ukatili na kuchangia amani na utulivu nchini.

 

Mpanju alisisitiza kuwa serikali inafanya uhakiki ili kuhakikisha uratibu wa mashirika unakuwa na ufanisi na pia ni matakwa ya sheria ya nchi. Aliongeza kuwa hakuna budi kuratibu shughuli zinazofanywa na NGO kwa kuwa kazi zinazofanywa ni kubwa.

 

Katika hatua nyingine, Mpanju aliwaagiza wasajili wasaidizi wa NGO kuwapitisha wadau kwenye miongozo mbalimbali ya NGO ambayo inaeleza serikali na sekta mbalimbali zinavyoshirikiana ili kufanya kazi kwa ufanisi.

 

"Nyie wasajili wasaidizi ndiyo wasimamizi wa sekta hii kwa niaba ya wizara, hivyo mnapokuwa na majukwaa kama haya, wapitisheni, hakikisheni mwongozo unasambazwa kwani ndio unatoa utaratibu mzuri wa namna ya kushirikiana bila migongano," alisisitiza.

 

Mmoja wa wadau wa NGO, Lediana Mng'ong'o, kutoka shirika la TAHEA alishauri mashirika ambayo yalikuwa yamesajiliwa kabla ya usajili wao kuhamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, yafutiwe na yasajiliwe upya kutokana na changamoto ya kulipa malimbikizo ya nyuma.

 

Naye Mtunza Hazina wa NaCONGO, John Kiteme, alisema baraza hilo linafanya kazi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha NGO zinafanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni, ikiwemo mchakato wa kusajili na kufuta mashirika.

 

Awali, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni, alisema mashirika yaliyosajiliwa mkoani hapa  ni 170 lakini yaliyo hai ni 91 na 79 yanasuasua kutokana na kutotekeleza malengo yao kwa mujibu wa usajili wao na kutokidhi matakwa ya sheria ikiwamo kutolipa ada na kutowasilisha taariza zao za utekelezaji.

Habari Kubwa