Ngono ya mdomo kichaka cha VVU

21May 2022
Sanula Athanas
MOROGORO
Nipashe
Ngono ya mdomo kichaka cha VVU

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya DARE, Dk. Lillian Benjamin, ameitaka jamii kuacha ngono ya mdomo kwa kuwa ni hatari kiafya, hasa kusababisha maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Amesema ute unaopatikana chini ya fizi na maji yaliyopo kwenye sehemu za siri za mwanamke, yamethibitika kitaalamu kuwa na VVU, hivyo kufanya ngono kwa mdomo kunaongeza uwezekano wa kuambukizwa virusi hivyo.

Akiwasilisha mada kuhusu uelewa wa VVU/UKIMWI wakati wa semina kwa wahariri na waandishi wa habari mjini Morogoro jana, Dk. Lillian alisema aina hiyo ya mapenzi ni hatari kwa kuwa mbali na kuchochea maambukizo ya VVU, wahusika wako hatarini kupata maradhi mengine.

"Ninashauri jamii iachane na aina hii ya ngono kwa sababu ni hatari kwa afya yao," Dk. Lillian alisema.

Nyangusi Laiser, Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), akizungumzia suala hilo, alisema: "Ngono ya mdomoni ni hatari kwa kuwa maji maji yaliyoko mdomoni yanaweza kuwa na chembe chembe za damu ikiwa mdomoni kuna michubuko, hivyo kama mtu ameambukizwa VVU, anaweza kumwambukiza mwenza wake VVU.

"Ikiwa ngono inahusisha mdomo kwenye via vya uzazi, kuna hatari ya kuambukizwa kupitia maji maji ya sehemu za siri za mwanamke," ofisa huyo alionya.Akirejea takwimu za kitaifa na kimataifa, Laiser alibainisha kuwa kwa mwaka 2020, kulikuwa na watu milioni 37.7 waliokuwa wanaishi na VVU duniani.

Kati yao, watoto wenye umri chini ya miaka 15 ni milioni 1.7 na kwamba asilimia 53 ya waliokuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi walikuwa wanawake.

Laiser alisema maambukizo mapya kwa mwaka 2020 yalikuwa watu milioni 1.5, kukionekana kuwapo kupungua kutoka watu milioni tatu mwaka 1997.

"Takwimu zinaonyesha kila siku takriban watu 4,000 huambukizwa VVU duniani na kati yao, 2,400 (asilimia 60) ni waliopo kusini mwa Jangwa la Sahara," alibainisha.

Kwa Tanzania, ofisa huyo alisema kuwa kwa mwaka 2020, watu waliokuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi walikuwa milioni 1.7.

"Maambukizo mapya mwaka 2020 nchini yalikuwa watu 68,000. Kati yao, 37,000 ni wanawake, wanaume 21,000 na watoto wenye umri chini ya miaka 15 wapatao 10,000.

 

Vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 wanaongoza kwa maambukizo mapya wakiwa asilimia 80," alibainisha.

Habari Kubwa