Wamesema wapo tayari kutafuta suluhu ila ushirikishwaji uwe wa dhati na usiwe na mashinikizo.
Akisoma tamko la madiwani 11 wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, vijiji 25 na viongozi wa mila wa Tarafa ya Ngorongoro, James Moringe, alisema sehemu kubwa haijashirikishwa na ripoti haikuzingatia maoni ya jamii.
Vile vile, alisema ripoti hiyo imependekeza eneo la wenyeji kutwaliwa, hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya jamii hiyo.
Moringe ambaye ni Diwani wa Kata ya Laitole (CCM), alieleza: "Sisi madiwani na Malaigwanani, kwa niaba ya wenyeji wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, kwa unyenyekevu tunamwomba Mheshimiwa Rais Magufuli atupie jicho eneo hili ili ikiwezekana abadilishe uongozi wa NCAA na kufumua taasisi hiyo kwa sababu imeshindwa kusimamia eneo na ndio chanzo cha mgogoro na kudorora kwa uhusiano kati ya jamii na wahifadhi."
Kabla ya kutolewa tamko hilo, Diwani wa Kakesio (CCM), Johannes Tiamasi, ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wafugaji nchini, alisisitiza kuwa wenyeji wako tayari kushirikiana na mamlaka katika kutatua matatizo yanayoikumba eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ikiwamo uvamizi wa mimea isiyo ya asili, ongezeko la idadi ya watu na maendeleo hafifu ya wenyeji.
"Shughuli za uhifadhi na za utalii zinachangia kwa sehemu kubwa kukuza uchumi wa nchi yetu na hivyo kupunguza umasikini. Wenyeji ni wahifadhi wa asili na wameendelea kuisaidia serikali katika kulinda, kutangaza na kushiriki kutatua matatizo yanayoikumba sekta ya maliasili na utalii," alisema Tiamasi
Aidha, Mwakilishi wa viongozi wa mila wa Tarafa ya Ngorongoro, Lazaro Saitoti, alimuomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damasi Ndumbaro asikubali pia kupotoshwa na akubali kukaa upya na wenyeji na kujadili namna ya kutatua matatizo yanayotajwa kuidhoofisha NCCA.
Saitoti alisema wenyeji wa Hifadhi ya Ngorongoro, si wavamizi wa eneo la hifadhi, bali ni wakazi halali wenye haki za msingi na wanaotambulika na sheria iliyoanzisha eneo hilo mwaka 1959.