Nguli aomba wadau hifadhi ya misitu kutoa elimu kwa wakazi wa Lindi

21Nov 2021
Christina Haule
Lindi
Nipashe Jumapili
Nguli aomba wadau hifadhi ya misitu kutoa elimu kwa wakazi wa Lindi

​​​​​​​WADAU wa uhifadhi wa misitu wa ndani na nje ya nchi wameombwa kujitokeza katika Wilaya ya Liwale mkoani Lindi ili kushiriki katika kutoa elimu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa sababu robo tatu ya Wilaya hiyo imebeba misitu inayohitaji kuhifadhiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Judith Nguli, amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea msitu wa kijiji cha Nambinda kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na wananchi katika usimamizi shirikishi wa mazao ya msitu kwa jamii (USMJ) chini ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa kushirikiana na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) waliofadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC).

Nguli amesema Wilaya hiyo imesheni utajiri mkubwa wa maliasili ikiwemo misitu hivyo wananchi wa Wilaya hiyo wanapaswa kupewa elimu ya kutosha kutambua umuhimu wa kuilinda na kuihifadhi sambamba na kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu ambazo haitahatarisha uwepo wake.

“Mbili ya tatu ya ardhi ya Wilaya ya Liwale imefunikwa na misitu, lakini kuna wadau wachache wa uhifadhi wilayani hapa wanaokuja kutuelimisha, sasa natoa wito kwa wadau wa uhifadhi kote nchini na hata nje ya nchi waje tushirikiane nao kwa pamoja kutoa elimu na mbinu za uhifadhi na matumizi endelevu ya mazao ya misitu” Amesema Nguli.

Aidha Nguli amepongeza juhudi za Uhifadhi wa misitu ya asili zilizofanywa na MJUMITA na TFCG kwa kusaidia kuhifadhi kwenye msitu wa asili wa kijiji cha Nambinda wilayani humo.

“Ninawapongeza kwa juhudi zenu kubwa za kuhakikisha misitu ya asili inahifadhiwa na rasilimali zake zinavunwa kwa njia endelevu…. Nilitamani mlichokifanya Kijijini Nambinda mngelifanya hivyo katika vijiji vingi zaidi wilayani hapa lakini ninawahakikishia kwamba tutaendelea kuunga mkono juhudi zenu katika suala hili la uhifadhi wa misitu” amesema Nguli.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema uongozi wa Wilaya umejipanga kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaobainika kuharibifu misitu ili kuilinda misitu hiyo isitoweke.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Liwale, Tina Sekamba, amesema wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 76 kati ya vijiji hivyo ni vijiji vitatu tu ambavyo havijapimwa na kuingizwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Sekamba amesema kuwa Halmashauri ya Liwale katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2021-22 imetenga jumla ya kiasi cha Shilingi 30 Milioni kwa ajili ya shughuli za uhifadhi wa misitu.

Naye Afisa Mawasiliano wa TFCG, Betty Luwuge amesema shirika la TFCG litaendelea kushirikiana na serikali za vijiji kutoa elimu na mbinu za uhifadhi endelevu wa misitu sambamba na matumizi bora ya ardhi yenye kujali na kuzingatia uvunaji wa rasilimali za misitu kwa njia endelevu.

Habari Kubwa