Nguo za mitumba kuanza kukamatwa mwezi ujao

22Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Nguo za mitumba kuanza kukamatwa mwezi ujao

NGUO za mitumba zilizo chini ya kiwango ambazo ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini, zitaanza kukamatwa kwenye maduka na masoko mbalimbali nchini kuanzia Julai mosi, mwaka huu.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage,

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema wamebaini uwapo wa nguo zilizo chini ya kiwango huku nyingine zikiwa kama chandarua na kwamba huo ni wizi wa fedha za wananchi.

"Haiwezekani kuona watu wachache wanaharibu soko kwa kuingiza bidhaa ambazo hazina vigezo. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani (FCC), wajiandae kutumbuliwa kama watashindwa kusimamia bidhaa zenye ubora kwani ndilo jukumu lao," alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mwijage alisema Jimbo la Giang Zu la nchini China, linatarajiwa kuwekeza Dola bilioni tano (sawa na Sh. trilioni 11) kwa miaka mitano kwenye sekta za viwanda.

Alisema kwa mwaka wa kwanza, Jimbo hilo litawekeza Sh. trilioni mbili ambazo zitafanya kazi pamoja na bajeti ya wizara hiyo.
Waziri Mwijage alisema ili kufanikisha upatikanaji wa viwanda vingi ndani ya nchi, lazima kuwapo kwa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi.

Alifafanua kuwa mbali ya uwekezaji huo wa Sh. trilioni 11, pia Serikali ya China imekubali kutoa Dola za Marekani milioni 100 (sawa na Sh. bilioni 220) kwa mwaka huu kwa ajili ya kuendeleza viwanda vidogo vidogo.

Pia alisema China imeelekeza Dola milioni 50 (sawa na Sh. bilioni 110) ambazo zitatolewa katika benki za biashara.
Hata hivyo, Waziri Mwijage alisema utaratibu unafanywa wa kuelekeza fedha hizo katika Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na Benki ya Maendeleo ya Wakulima Tanzania (TADB).

Aidha, Waziri Mwijage alisema Kituo cha Kibiashara Kurasini (Kurasini Logistic Center) kinachotarajiwa kuanzishwa kitasaidia kuwapunguzia wafanyabiashara safari za nje bidhaa na badala yake shughuli yote hiyo itaratibiwa mahali hapo.Alitaja moja ya manufaa ya kituo hicho cha Kurasini ni kutoa ujuzi na ajira kwa Watanzania.

"Napenda kusisitiza kuwa kinachotokea baada ya kufanikisha mradi huo, vijana wengi wataweza kuunganisha bidhaa wenyewe hivyo kuongeza ajira, tutakuwa na wawekezaji kutoka China, Austria, Uingereza na nyingine ambapo hadi sasa tumeshatoa Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi," alifafanua.

Habari Kubwa