NHC yaombwa kuifikia mikoa mipya

04Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Simiyu
Nipashe
NHC yaombwa kuifikia mikoa mipya

WANANCHI wameliomba Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kuifikia mikoa mipya kwa lengo la kutatua changamoto ya nyumba na makazi kwa watumishi na wananchi wa maeneo hayo.

NYUMBA ZA NHC. PICHA NA MITANDAO.

Wananchi hao wameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti  baada ya kutembelea banda la shirika hilo katika maonyesho ya wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Aidha NHC wametakiwa kuongeza nguvu kuhakikisha wanafanya uwekezaji katika mikoa hiyo ili kupunguza adha kwa watumishi wa umma na wakazi wa maeneo hayo kupata nyumba bora na za kisasa kwa ajali ya kupanga.

‘’Shirika la nyumba kwa mkoa wetu huu bado ni changamoto kwa watumishi kwani hawana mahala pa kukaa kwa sababu watumishi wengine kipato chao ni kidogo sana na hawawezi kumudu gharama za upangaji…shirika hili liangalie hii mikoa mipya, zipatikane nyumba za kuishi watumishi, wengine wanakata tamaa ya kazi kutokana na ukosefu wa makazi’’  amesema, Nestory Mazinzi mkazi wa Simiyu

Naye Anthony Solo mkazi wa Shinyanga, amesema kuwa NHC wamefanya kazi kubwa katika ujenzi wa nyumba bora lakini limejikita zaidi mjini na kuwataka pia kuwekeza katika mikoa mipya inayokuwa kwa haraka ambayo inapokea wageni wengi kila wakati ukiwemo mkoa wa Simiyu ambao umekuwa na matukio ya kitaifa kila wakati.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa NHC, Levinico Mbilinyi amesema kwa sasa shirika hilo linatarajia kutekeleza mradi Jijini Dodoma wa nyumba 1,000 za makazi ambapo utakuwa ni mradi wa nyumba za bei nafuu na zitajengwa kwa lengo la kuuzwa na kupangishwa.

‘’Nyumba hizi 1,000 zitajengwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza tutajenga nyumba 400 na awamu ya pili na ya tatu tutajenga nyumba 325 na 275 sambamba na hilo tuna mradi mkubwa wa viwanja katika jiji la Arusha lakini lengo kubwa ni kuifikia kila wilaya nchini’’amesema Mbilinyi

Habari Kubwa