NHC yapewa mchongo uwekezaji mji Kahama

27Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Shinyanga
Nipashe
NHC yapewa mchongo uwekezaji mji Kahama

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetakiwa kufanya uwekezaji wa majengo ya biashara na nyumba za kupangisha katika mji wa Kahama kutokana na mji huo kuendelea kukua kwa kasi.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula, alitoa kauli hiyo juzi wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Shinyanga kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi inayosimamiwa na NHC.

Alisema Kahama ni mji unaokua kwa kasi kubwa na kama NHC haijafikiria kuwekeza katika mji huo, ijipange kuona namna gani inaweza kutumia fursa ya kukua huko kwa mji kwa kufanya uwekezaji na kusisitiza kuwa hata kama hakuna uhitaji wa nyumba za kuuza, shirika linaweza kujenga majengo ya biashra yanayoweza kupangishwa.

"Uwekezaji wowote mtakaoufanya hapa Kahama kama hakuna walioonyesha dhamira ya dhati ya kununua basi jengeni nyumba za kupanga ili kuwa na nyumba za kutosha mji unakuwa haraka," alisema Dk. Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, kila mahali ambapo NHC imewekeza katika majengo ya kibiashara hakuna sehemu imekosa wapangaji na kadri mji wa Kahama unavyokua kwa kasi, bado NHC inaweza kufaidika.

Alimwagiza Meneja wa NHC Mmkoa wa Shinyanga kufanya uamuzi ya haraka kwa lile eneo lililoainishwa na Manispaa ya Kahama kwa kwa ajili ya uwekezaji na kusisitiza kuwa Kahama bado inazo fursa nyingi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili, Clemence Nkusa, alimwambia Naibu Waziri kuwa tayari halmashauri yake ilishatenga eneo kwa ajili ya shirika hilo kufanya uwekezaji.

Kutokana na hatua hiyo, Naibu Waziri Mabula aliitaka NHC kufanya uamuzi wa haraka na kufikia Desemba, mwaka huu, wizara iwe imepata taarifa ya aina ya uwekezaji utakaofanyika.

Dk. Mabula pia aliitaka NHC kufikiria namna ya kufanya uwekezaji wa nyumba katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu kutokana na kuwa na uhitaji wa nyumba, zikiwamo za watumishi.

Habari Kubwa