NHC yatangaza kibano wakwepa kodi wake 265

25Mar 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
NHC yatangaza kibano wakwepa kodi wake 265

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limetoa mwezi mmoja kwa wapangaji wake 265 nchini waliohama na wanaoendelea na upangaji kulipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Tangazo lililotolewa na NHC katika gazeti hili jana, liliwataka wadaiwa wote waliohama na wanaoendelea kuishi wameacha deni la Sh. trilioni 1.399.

Taarifa hiyo ilitaja wapangaji waliohama na kuacha madeni katika mikoa husika na kiasi wanachodaiwa kuwa ni Arusha Sh. bilioni 9.253, Dodoma Sh. bilioni 5.606, Ilala Sh. bilioni 964, Iringa Sh. bilioni 1.992 na Kigoma Sh. milioni 399.

Mingine ni Kilimanjaro Sh. bilioni 15.973 na Kinondoni Sh. bilioni 115.462.

Mikoa mingine ni Lindi Sh. bilioni 14.892, Mara Sh. bilioni 1.117, Mbeya Sh. bilioni 15.979, Morogoro Sh. bilioni 2.168, Mtwara Sh. bilioni 4.086, Tanga Sh. bilioni 15.401 na Temeke Sh. bilioni 232.928.

“Shirika linatoa rai kwa kila anayedaiwa kuhakikisha amelipa madeni yake ili kuepuka usumbufu utakaoweza kujitokeza kwa kutangazwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Ni matumaini yetu kuwa wadaiwa wote watatimiza wajibu wao wa kulipa madeni yao bila usumbufu,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa ilifafanua kuwa, wataendelea kuwatangaza wadaiwa sugu wote waliohama na wanaoendelea na upangaji hadi hapo madeni yao yote yatakapokuwa yamelipwa.

Habari Kubwa