NHIF yaonya madaktari, wauguzi

20Feb 2017
Anceth Nyahore
BARIADI
Nipashe
NHIF yaonya madaktari, wauguzi

MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda, amewaonya wauguzi na madaktari katika zahanati, vituo vya afya na hospitali hapa nchini wenye tabia za ubaguzi kwa wagonjwa wanaotibiwa kwa mfuko huo.

MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda.

Aidha, Makinda amesema vituo vya afya, zahanati na hospitali zitakazobainika kufanya ubaguzi huo, zitaondolewa usajili wa NHIF.
Alitoa onyo hilo alipokuwa akizungumza katika kikao cha wadau wa NHIF Mkoa wa Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini hapa mwishoni mwa wiki.

Makinda aliwataka madaktari na wauguzi sasa kubadilika na kuzingatia taratibu zote za utoaji wa huduma za afya katika sehemu zao ya kazi.

Alisema watumishi wa vituo vya afya vya serikali, ndivyo vinavyoongoza kwa wahudumu wake kutoa huduma zisizofaa kwa wagonjwa wanaotumia NHIF na kuwataka kubadilika kwa kuwa wanapoteza hadhi ya vituo hivyo.

Makinda ambaye ni Spika wa Bunge mstaafu wa Bunge la Jamhuri, alisema tabia mbaya zinazofanywa na baadhi ya wataalamu hao
wa afya za kuwafanyia ukatili wa kuwanyanyasa wagonjwa wanachama wa NHIF, hazikubaliki na lazima zikome kwani zinawafanya wakose imani na huduma inayotolewa na mfuko huo.

“Kuna ukatili wanafanyiwa wateja wetu wanaotumia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wanapofika katika vituo vya afya kupata huduma kwani hunyanyaswa sana," alisema Makinda.

“Kuanzia sasa, vituo vitakavyobainika vikiendelea na tabia hiyo, hatutasita kuondoa huduma hiyo na kuvifutia usajili wa kutoa huduma za NHIF na niwakumbushe wahudumu wa afya kuwa wema wako kwa mgonjwa, ni nusu ya dawa utakayompatia na kumfanya apone maradhi yanayokamkabili,”alisema Makinda.

Alisema NHIF inavihudumia na kutoa vifaa tiba na dawa za aina mbalimbali vituo vya afya kwa mujibu wa taratibu, lakini bado kumekuwa na malalamiko ya wanachama wanapokwenda kutibiwa kwani hukutana na vikwazo na kujiona kama wamepotea njia kwa kutumia NHIF.

Naye Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema zipo taarifa za wauguzi na madaktari wanaowanyanyapaa wagonjwa wanaotumia huduma za Mfuko.

Mtaka akiwa Mkuu wa Mkoa, kamwe hatakubali jambo hilo lifanyike na atakayejaribu kufanya hivyo, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Alisema serikali ina mpango wa kuhakikisha kila Mtanzania anaingia kwenye mfumo huo na wanaokwamisha ni vema wakachukuliwa hatua.

Aidha, Mtaka alisema mikakati ya mkoa kwa sasa ni pamoja na kujenga maduka makubwa ya dawa ya serikali katika halmashauri zote za mkoa ili kupunguza malalamiko ya wananchi kuwa na upungufu wa dawa katika vituo vya afya vya serikali.

Kwa upande wake, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humu, imeahidi kuwa kuanzia sasa itafuatilia kwa karibu malalamiko yote yanayotolewa dhidi ya mwenendo wenye harufu ya rushwa katika utoaji wa huduma kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitali.

Habari Kubwa