Ni huzuni, majonzi, simanzi

24Sep 2018
Na Waandishi Wetu
Dar es salaam na Mwanza
Nipashe
Ni huzuni, majonzi, simanzi

HUZUNI, majonzi na simanzi vilitawala jana katika kijiji cha Ukara wakati miili ya watu tisa waliofariki katika ajali ya MV. Nyerere Alhamisi wiki iliyopita, ikizikwa.

waombolezaji wakiwa katika eneo maaalum katika kijiji cha ukara walipozikwa watu waliofariki akatika ajali ya kuzama kwa kivuko cha mv. nyerere.

Katika ajali hiyo watu 224 walifariki na wengine 41 kuokolewa baada ya kivuko hicho kuzama katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kufika katika gati ya bandari ndogo ya Ukara, kikitokea Bugorora.

Shughuli ya kuzika miili hiyo ilifanyika jana katika kijiji cha Ukara majira ya saa 8 mchana na kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, iliyotawaliwa na vilio na simanzi.

Akizungumza na wananchi waliokusanyika kwenye mazishi hayo, Majaliwa alisema kuzama kwa kivuko hicho ni tukio la kusikitisha na limeacha majonzi makubwa kwa Watanzania wote.

"Mpaka sasa vifo vimefikia 224 na kati ya hiyo, wanawake ni 125, wanaume ni 71 watoto wa kike ni 17 na wakiume ni 10 na miili minne ambayo haijatambuliwa tumechukua vipimo vya DNA, ili ndugu zao wakijitokeza waweze kufanyiwa uchunguzi kama vinasaba vyao vinaendana na marehemu hao,” alisema Majaliwa.

Alisema ajali hiyo imesababisha wapendwa wengi kufariki na kuacha huzuni, vilio kwa wananchi wengi.

“Ni tukio la kusikitisha, limetuachia majonzi, ajali hii imesababisha wapenzi wetu kututoka, hivyo ni msiba wa Watanzania wote,” alisema Majaliwa.

Aliwataka Watanzania kuwa watulivu, kwa kuwa serikali imeishaanza kuchukua hatua na tayari maofisa wote wakuu wanaohusika na kivuko hicho wanashikiliwa kwa mahojiano.

Aidha, alisema serikali imeshachukua hatua ya kuleta kivuko mbadala ambacho kitafanya huduma zake kama kawaida katika gati la Bugorora na Ukara, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku.

Waziri Mkuu pia alisema serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha usafiri wa majini katika bahari na Ziwa Victoria katika mialo 140, ikiwamo Bezi, Bukondo, Kayenze na Senga kwa kuwekewa kivuko, huku akitoa wito kwa Watanzania kushirikiana na ndugu wa marehemu kwa kuwafariji zaidi badala ya kuwajaza maneno mabaya ambayo yatavuruga amani.

Majaliwa pia alishuhudia uvutwaji wa kivuko hicho utakaochukua wiki moja ambao unafanywa na wataalamu kutoka Songoro Marine kwa kushirikiana na Tamesa kwa kutumia mtambo kutoka kampuni ya Nyanza Road.

Akitoa taarifa za uendeshaji wa maafa hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya maafa, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe, alisema kivuko hicho kilitengenezwa mwaka 2004 kikiwa na uwezo wa kubeba abiria 101 tani 25 na magari matatu.

Akizungumza kwa niaba ya wafiwa, Peter Mgaya, alisema ajali hiyo imeacha vilio kila nyumba kwa kuwa ni asilimia kubwa ya wakazi wa Ukerewe wameondokewa na wapendwa wao.

“Kwa niaba ya waliofiwa ninaomba ushirikiano uliotokea leo (jana) uendelee, tushirikiane katika wakati huu mgumu,” alisema Mgaya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha, aliiomba serikali kupeleka boti za kisasa katika kisiwa cha Ukerewe kwa kuwa zinazotumika sasa zimetengenezwa kwa mbao.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba kivuko cha uhakika kitakacho wasafirisha wananchi kwa uhakika, vivuko vinavyotumika huku vingi vimetengenezwa kwa mbao,” alisema Nyamaha.

*Taarifa hii imeandaliwa na Rose Jacob, Mwanza na Gwamaka Alipipi, Dar

Habari Kubwa