NI KITIMTIM

20Dec 2016
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
NI KITIMTIM
  • WANANCHI wapuuza risasi, mabomu na kuchoma moto kituo cha polisi
  • ASKARI walazimika kutimua mbio, wanne wajeruhiwa kwa kupigwa mawe
  • RAIA auawa katika mapambano, wengine watatu wakimbizwa hospitalini
  • YADAIWA chanzo hasira za wananchi kutaka wapewe watuhumiwa wa mauaji

MTU mmoja ameuawa, na wengine saba kujeruhiwa katika mapambano makali kati ya wananchi na Jeshi la Polisi wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.

Katika mapambano hayo, pia kituo cha polisi kilichomwa moto, wananchi kadha na polisi kujeruhiwa.

Chanzo cha mapambano hayo kimeelezwa kuwa ni wakazi wa Mamlaka ya Mji wa Makongolosi wilayani Chumya kugombea watuhumiwa wa mauaji.

Habari zinaeleza kuwa watu wawili walimuua mtu mmoja kwa tuhuma za ushirikina na baada ya polisi kuwakamata na kuwashikilia ndipo wananchi waliokuwa na hasira wakaenda kituoni kutaka kuwaua.

KITUO CHA POLISI CHACHOMWA
Baada ya kukivamia Kituo cha Polisi Makongolosi walikichoma moto na kuharibu baadhi ya mali zilizokuwapo zikiwamo pikipiki, mbao na magogo yaliyokuwa yamehifadhiwa kituoni hapo.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya mchana na kwamba polisi walikwenda kuwakamata watu wawili waliokuwa wanahisiwa kuhusika katika mauaji ya Jacob Brown (66) kwa sababu za imani za kishirikina.

MKASA MZIMA
Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji hayo ni Erasto Robert (26) na Basi Linus (24).

Alisema walikamatwa kwa tuhuma za kumvamia Brown nyumbani kwake nyakati za usiku akiwa amelala kisha kumuua kwa kumkata na vitu vyenye ncha kali.

Kamanda Kidavashari alisema kuwa baada ya Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa hao na kuwapeleka katika kituo cha Makongolosi, wananchi wa mji huo walipeana taarifa na kuhamasishana kwenda kuwapora watuhumiwa hao mikononi mwa polisi ili na wao wawaue kama njia ya kulipiza kisasi.

Alisema kuwa taarifa hizo zilisambaa haraka hali iliyowafanya wananchi zaidi ya 500 kukusanyika na kuwaamrisha askari kuwashusha watuhumiwa hao ili wawaue, hali iliyowafanya askari kuwatawanya wananchi hao kwa kutumia mabomu ya machozi.

Alisema baada ya askari kuona wanazidiwa, waliamua kukimbia na watuhumiwa hao kuelekea upande wa Lupa na ndipo wananchi hao walipoamua kufunga njia kwa mawe upande wa kutokea Chunya mjini na upande wa Lupa kisha kuendeleza fujo.

Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, wananchi hao pia walichoma magurudumu katika milango ya kituo cha polisi na kuvunja milango na madirisha na ndipo polisi walipoamua kuomba msaada kutoka Chunya mjini na Mbeya.

Alisema kuongezeka kwa idadi ya askari kulisaidia kuwasambaratisha wananchi hao na vurugu kuzimwa.

Alimtaja aliyepoteza maisha katika vurugu hizo kuwa ni Amoke Mbilinyi (25) ambaye alifariki dunia wakati akikimbizwa hospitalini.

MAJERUHI
Waliojeruhiwa ni Domita Mwangamila (24), Amos Kandonga (16) na Hawa Masumbuko (21).

Majeruhi wengine ni askari wanne ambao ni G. 4684 PC. Deogratius, H. 2361 PC. Shaban, H. 5314 PC. Ashel na H. 3650 PC. Adamu ambao walijeruhiwa na wananchi hao waliokuwa wanakabiliana na askari kwa kuwarushia mawe.

41 WATIWA MBARONI
Alisema kuwa watuhumiwa 41 walikamatwa katika tukio hilo na kwamba 23 walifikishwa mahakamani jana huku wengine wakitarajiwa kufikishwa siku chache zijazo.

Kamanda Kidavashari aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa maelezo kuwa ni kinyume cha sheria za nchi.

Habari Kubwa