Ni mafuriko ubunge CCM

15Jul 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ni mafuriko ubunge CCM

NI Mafuriko. Ndicho kinachoonekana katika uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali nchini.

Waliojitokeza wengi ni waliowahi kuwa wabunge kwenye majimbo hayo kipindi kilichopita, waliokuwa wabunge hadi Julai, mwaka huu, mawaziri, naibu mawaziri, wanasheria, wasomi na wanataaluma mbalimbali.

Pia katika mchakato huo, wamo waandishi wa habari, wafanyabiashara, wakuu wa zamani wa taasisi nyeti, vijana na viongozi wa ngazi mbalimbali za serikali wakiwamo waliokuwa wakuu wa mikoa.

Licha ya mamia ya watu kupigana vikumbo kuwania ubunge majimboni kutoka katika makundi hayo, yako majimbo ambayo yametia fora kwa wingi wa watu likiwamo la Kibamba ambalo hadi jana lilikuwa na wanachama 88 waliochukua fomu. Jimbo hilo kabla ya kuanza mchakato, lilikuwa chini ya John Mnyika kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katibu wa CCM wilaya ya Ubungo, Sylvester Yeredi, alisema wagombea wa kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugomba katika majimbo ya Ubungo na Kibamba walianza kumiminika kuanzia saa 2:00 asubuhi.

Jimbo lililofuata kwa kuvunja rekodi ni Ubungo ambalo kuna wagombea 65. Mbunge wa Jimbo hilo katika kipindi kilichopita alikuwa SAEED Kubenea wa CHADEMA.

Katika wilaya ya Kinondoni yenye majimbo mawili ya Kawe na Kinondoni, Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, Sure Mwasanguti, alisema waliochukua fomu kwa jana walikuwa 80 kwa jimbo la Kawe na Kinondoni 31

Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Iddi Mkoa, alitanabahisha kuwa katika jimbo la Segerea waliochukua fomu alikuwa 41, Ukonga 50 na Ilala tisa.

MAWAZIRI WAJITOSA

Katika kinyang’anyiro cha ubunge, mawaziri sita walichukua fomu jana. Mawaziri hao ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (Buhigwe), Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dk. Joyce Ndalichako (Kasulu Mjini), Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Vwawa), Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (Karagwe), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Suleiman Jaffo ambaye anaomba ridhaa tena Kisarawe.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Palamagamba Kabudi (Kilosa) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki aliyejitosa jimbo la Same Magharibi.

Katika kundi hilo pia wamo naibu mawaziri Dk. Agelina Mabula wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi (Ilemela) na wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji Kondoa Mjini.

SPIKA NA NAIBU WAKE

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania katika bunge lililovunjwa, Job Ndugai, amejitokeza kuomba tena ridhaa katika jimbo la Kongwa huku naibu wake, Dk. Tulia Ackson, akichukua fomu kuomba ridhaa ya kugombea jimbo la Mbeya Mjini ambalo mbunge wake alikuwa Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu.

Aidha, wabunge wa zamani ambao katika uchaguzi mkuu uliopita waliangushwa ama kwenye uchaguzi mkuu au wakati wa kura za maoni wamechukua fomu kujaribu kurudi tena.

Baadhi ya wabunge hao ni aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya tatu na ya nne, Prof. Juma Kapuya (Kaliua) na Abbas Mtemvu, Temeke.

Mbali na wabunge hao wa zamani, kinyang’anyiro cha ubunge pia kinawahusisha waliokuwa wakuu wa mikoa ambao hivi karibuni, ama walitenguliwa au kustaafu. Mmoja wa hao ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliyechukua fomu kugombea Arusha Mjini.

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali (mstaafu) Emmanuel Maganga anayewania Mvomero na Aggrey Mwanry (Tabora) anayewania kurejea Siha baada ya kuangushwa katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Pia, wamo viongozi wa dini kama Josephat Gwajima wa Kanisa ya Ufufuo na Uzima aliyejitosa jimbo la Kawe na Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. James Jesse, ambaye amechukua fomu Segerea.

Wengine waliojitokeza ni Frederick Lowassa ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited, Francis Nanai, ambaye ni miongoni mwa waliojitosa katika jimbo la Kawe.

WANAHABARI WAMO

Katika safu ya waliojitokeza kugombea ubunge, pia wamo wanahabari akiwamo mwandishi wa IPP Media Morogoro, Idda Mushi, anayewania Moshi Vijijini.

Waandishi wa habari wengine waliojitokeza ni Zamaradi Mketema (Kawe), Andrew Kuchonjoma (Songea Mjini), Cyprian Musiba (Mwibara), Tumaini Msowoya (Viti Maalum Iringa) na Hamisi Mkotya (Chemba).

Habari Kubwa