Ni Majonzi

27Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ni Majonzi

MKURUGENZI wa Vipindi wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba, amefariki dunia jana usiku nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.

Ruge alipelekwa nchini humo mwishoni mwa mwaka jana kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya figo.

Kutokana na kifo hicho, Rais John Magufuli, jana usiku alituma salamu za rambirambi kwa familia yake na kusema amepoteza kijana wake muhimu katika tasnia ya habari nchini.

Rais Magufuli katika rambirambi hiyo aliyoitoa pia kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa ‘Tweeter’ alisema: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kijana wangu Ruge Mutahaba. Daima nitakukumbuka kwa mchango wako mkubwa katika tasnia ya habari, burudani, na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana.Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina.”
Taarifa za msiba Ruge zilitangazwa rasmi na Millad Ayo katika kipindi cha Amplifier kikiendelea Clouds jana usiku.

Wakati Ayo akiendelea na kipindi hicho ndipo taarifa za msiba huo zilipokuja na kulazimika kutangaza kuwa, kipindi hicho kimeishia wakati huo baada ya kupata taarifa za msiba huo.|

“Tunaomba radhi kwa sasa kipindi cha Amplifier kwa leo kitaishia hapo tumepata taarifa za kushtusha ambazo zimemjeruhi kila mmoja humu ndani na kubadilisha hali ya hewa,” alisema na kuongeza:

“Mmoja wa waasisi na Mkurugenzi wa wa vipindi na uzalishaji Clouds Media Group Ruge Mtahaba ametutoka leo (jana) huko Afrika Kusini alikokuwa amekwenda kwa matibabu, mioyo yetu imejeruhiwa sana tutaendelea kuwapa taarifa zote, pumzika kwa amani” alimaliza.

Mmoja wa wafanyakazi wa Clouds, Hassan Ngoma, aliiambia Nipashe kwamba msiba wa Ruge uko Mikocheni karibu na shule ya Fezza nyumbani kwa baba yake mzazi.

Alisema taarifa walizozipata ni kuwa Ruge alifariki jana saa moja jioni.

Jumatatu iliyopita, mdogo wa Ruge, Mbaki Mutahaba, akihojiwa kwenye kipindi cha 360 cha Clouds TV, alisema Ruge alianza kuumwa mwaka jana.

Akizungumza kwenye kipindi hicho Mbaki alisema gharama za matibabu Afrika Kusini ni kubwa kwa siku inaweza kufikia Sh. milioni tano hadi sita na hadi wakati huo zaidi ya Sh. milioni 600 zilikuwa zimeshatumika.

Kuhusu historia ya kuumwa kwake, Mbaki alisema Ruge alianza kuumwa mwaka jana na kabla ya kupelekwa Afrika Kusini alilazwa Hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es Salaam na baadaye alipelekwa nchini India.

“Jopo la madaktari kutoka hosptali ya Kairuki na Muhimbili wakasema apelekwe Afrika Kusini kwa sababu ni karibu ila matibabu ya huko yana gharama kubwa,” alisema na kuongeza;

“Ila msaada ni kubwa ukianza na mheshimiwa Rais Magufuli, alishatoa msaada mkubwa sana na anakuwa akipiga simu kujua hali yake kila wakati ila kule gharama ya matibabu ni kubwa kwa siku inaweza kufika milioni tano mpaka sita.” alibainisha.

Mbaki alisema mwezi Aprili mwaka jana, alianza kuumwa bila kujua ni tatizo la figo na mwezi uliofuata ndipo alipopata majibu ya hospitali kuwa anasumbuliwa na figo.

Alisema baada ya kufika India, walimwambia figo zake hazina ulazima wa kubadilishwa.

“India hakukaa muda mrefu alirejea Tanzania na kuendelea na matibabu, lakini baadaye hali ikabadilika mara ya pili akalazwa Kairuki, kutokana na hali yake ilivyokuwa ilipofika mwezi Septemba mwaka jana madaktari wakapendekeza apelekwe Afrika Kusini,” alisema.

Alisema baada ya kufika Afrika Kusini mambo mengine yakaibuka yanayohusiana na figo, hivyo madaktari wakawa wanatibu siyo tu figo na mengine.

“Katika kipindi chote alichokwenda tangu Septemba hadi sasa madaktari wamekuwa wakitibu siyo tu masuala ya figo wakati mwingine presha,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Kinachotia moyo yale yaliyokuwa yanasababishwa na figo yametulia, changamoto ni kumrudisha kwenye hali yake ya kawaida kwa sababu amekaa hospitali muda mrefu hivyo kwa sasa amekuwa mgonjwa wa kumsaidia kupata nafuu, hali yake siyo mbaya inaridhisha ikilinganishwa na awali,” alisema.

Habari Kubwa