Ni shangwe bajeti 2021/22

11Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Ni shangwe bajeti 2021/22

NI shangwe! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya serikali kuwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha ikipunguza tozo na kodi kwenye maeneo mbalimbali.

Mapendekezo hayo yaliyowasilishwa jana na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, yanahusisha kupunguza Kodi ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE) kwenye mishahara, kupunguza kodi kwenye mazao ya kilimo cha mboga na maua, urasimishaji wa ardhi na nyasi bandia zinazoingizwa nchini kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya michezo.

Punguzo la kodi na tozo pia linapendekezwa kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambayo serikali imependekeza kufuta ongezeko la asilimia 10 kila mwaka katika deni la mnufaika, huku tozo kwa madereva bodaboda na bajaj ikipendekezwa kushushwa kutoka Sh. 30,000 hadi Sh. 10,000.

Serikali pia inapendekeza kuweka utaratibu wa kisheria kwa posho za madiwani kulipwa na Hazina kupitia akaunti zao moja kwa moja na kuwe na posho maalum kwa maofisa tarafa na watendaji wa kata.

Mapendekezo hayo pia hayajawaacha nyuma wastaafu, serikali ikitarajia kutenga fungu maalum la kulipa madeni yao na kupandisha madaraja watumishi wa umma.

Katika bajeti hiyo, serikali inatarajia kutumia zaidi ya Sh. bilioni 300 kugharamia Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022, huku kodi ya majengo ikipunguzwa.

Waziri Nchemba alisema maeneo mahususi ambayo serikali imelazimika kuongeza bajeti ni yanayolenga kugusa wananchi moja kwa moja zikiwamo sekta za maji, nishati na afya.

Kodi inapendekezwa kuongezwa kwenye michezo ya kubahatisha kwa lengo la kupata fedha zitakazotunisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo.

Kwa ujumla, mapendekezo hayo ya serikali yanaonekana kulenga kulinda bidhaa za ndani, suala hilo likiakisiwa na uamuzi wa kuongeza kodi na tozo kwenye bidhaa nyingi kutoka nje huku za ndani zikipunguziwa.

Habari Kubwa