Ni utata mtupu

09Dec 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Ni utata mtupu
  • MASWALI KIBAO MIILI 6 ILIVYOKUTWA KWENYE VIROBA MTONI RUVU

WAKATI Jeshi la Polisi likianza uchunguzi mkali kuhusiana na undani wa tukio la kukutwa kwa miili sita ya vijana wa kiume iliyokutwa kandoni mwa Mto Ruvu mkoani Pwani, maswali kibao yameibuka kuhusiana na utata wa jambo hilo.

Miili ya watu hao wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 15 na 25 iliopolewa kwa nyakati tofauti katika eneo moja la Mto Ruvu juzi na kukutwa ikiwa tayari imeanza kuharibika huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi akieleza kuwa askari kadhaa wamepelekwa katika eneo la tukio ikiwa ni sehemu ya uchunguzi kabambe waliouanza ili kubaini undani wa suala hilo.

Utambuzi wa majina ya wahusika; mahala wanakotoka, nani wanahusika na mauaji na ilikuwaje miili hiyo ikanusurika na mashambulizi ya mamba waliomo kwenye Mto Ruvu ni baadhi ya maswali yanayotarajiwa kujibiwa kupitia uchunguzi huo wa Polisi kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.

Aidha, maswali mengine yanayoibua utata wa vifo hivyo ni pamoja na kujua kama kwenye mto huo kuna miili ya watu wengine zaidi; sababu za miili ya wafu kuwa ni ya jinsia ya kiume pekee; ilikuwaje wakakutwa katika eneo moja la mto, ni lini waliuawa;

wapi na kwa nini hadi sasa hakuna taarifa za kuwapo kwa ndugu wanaotafuta jamaa zao wenye wajihi sawa na wa marehemu.

Kwa mujibu wa Kamanda Mushongi, wafu hao walikutwa mtoni kwa namna ya kushangaza kutokana na ukweli kuwa kila mwili ulikuwa umefungwa ndani ya mfuko wa sandarusi na kushonwa juu huku pia ikifungwa pamoja na jiwe kubwa.

Tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Mtoni Darajani, Kata ya Makurunge, Wilaya ya Bagamoyo, Pwani na kuzua taharuki kwa wakazi wa kitongoji hicho.

Katika tarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, Kamanda Mushongi alisema kutokana na miili ya marehemu hao ilivyoharibika, inaashiria kuwa ilisafirishwa kwa maji umbali mrefu.

Alisema kati ya Desemba 6 na 7 mwaka huu, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema wanaojishughulisha na kilimo na uvuvi kwenye Mto Ruvu kwamba wameona miili ya watu hao ambao hawajulikani ikiwa inaelea majini.

Alisema kuwa polisi walipofika eneo la tukio walibaini miili ya watu hao ambao wote ni wanaume na hadi sasa bado hawajatambulika.

"Kutokana na miili hiyo kuharibika vibaya, ilifanyiwa uchunguzi na daktari na kuamriwa izikwe," alisema Kamanda Mushongi na kuongeza:

"Tunaendelea na ufuatiliaji kujua miili hiyo ilitokea wapi hadi kufikia kukutwa kwenye mkoa wetu kwa kuwa inaonyesha ilisafirishwa kwa maji umbali mrefu kutokana na namna maiti hizo zilivyokuwa zimeharibika."

Diwani wa Kata ya Makuruge, Paul Kabile, aliiambia Nipashe juzi akiwa katika eneo la tukio kwamba miili hiyo ilikutwa ikiwa kila mmoja kwenye mfuko wa sandarusi na kufungwa jiwe, hali iliyowaacha katika mshangao mkubwa.

MASWALI MAGUMU
Wakizungumza na Nipashe kwa sharti la kutoandikwa majina yao, baadhi ya wakazi walihoji namna miili hiyo ilivyosalimika kutokana na kuwapo kwa mamba wakali katika baadhi ya maeneo ya Mto Ruvu kabla ya kukutwa juzi.

Aidha, swali jingine ni kuhusiana na hofu kuwa pengine kuna miili mingine zaidi ya hiyo ambayo bado haijaonekana na hivyo, ni wazi kwamba Jeshi la Polisi litakuwa na kazi ya ziada kujiridhisha zaidi.

“Je, kulikoni wafu hawa ni wa jinsia moja ya kiume pekee? Ilikuwaje wakakutwa eneo moja? Waliuawa lini na wapi? Kwa nini waliuawa na kina nani wanahusika?” Mmoja wa watu waliozungumza na Nipashe alihoji.

Kadhalika, swali jingine ni kwa nini hadi sasa hakuna watu waliojitokeza kuwatafuta ndugu zao, hilo likitokana na ukweli kuwa miili ya marehemu hao ilionekana kuharibika baada ya kuwa majini kwa siku kadhaa.

Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa kwa namna inavyooneka, upo uwezekano kuwa marehemu hao ni miongoni mwa vijana kadhaa wa kigeni wanaoingia nchini kwa njia haramu, hasa ile ya kubebwa kwenye malori ya mizigo na kufa njiani kwa ukosefu wa hewa na sababu mbalimbali; hali inayowalazimu wanaowaleta kujiepusha nao kwa kuwatupa mbali wawezavyo ili wasipatikane.

“Walikutwa kwenye viroba huku wamefungiwa na mawe… ni wazi kwamba waliowatupa hawakutaka miili hii ionekane na mtu,” chanzo kiliiambia Nipashe.

Aidha, chanzo kingine kilieleza kuwa uchunguzi wa Polisi ndiyo tegemeo pekee la suala hilo kwa sababu upo pia uwezekano kuwa kuna watu wamefanya unyama wa kuwaua watu wasio na hatia na kuwatupa mtoni kwa nia ya kupoteza kabisa ushahidi.

KAMANDA AFUNGUKA ZAIDI
Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda Mushongi alisema hawalali na tangu juzi askari polisi wamepiga kambi kando ya Mto Ruvu ili kubaini kama kuna miili mingine zaidi na pia kujua ukweli wa kile kilichotokea.

Alisema hadi jana saa 12:00 jioni walikuwa wakiendelea na uchunguzi zaidi kwenye eneo la tukio na kwingineko kwenye maeneo ya mto, lakini hawakubaini kuwapo kwa miili hiyo mingine.

Aidha, alisema kuwa uchunguzi wao unaendelea na hadi sasa bado wanatafuta majibu ya maswali mengi kuhusiana na jambo hilo kabla ya kuchukua hatua nyingine zaidi.

"Bado hatujajua miili ilitoka wapi na ilitupwa na nani… ilikuwa imeharibika vibaya, ikabidi daktari aruhusu izikwe haraka," alisema na kuongeza:

"Ilikuwa si rahisi kugundua lolote kwa hali ile. Hiki ni kitendawili. Askari wamepiga kambi Mto Ruvu kufuatilia na kujua kama kuna miili mingine zaidi."

*Imeandikwa na Magreth Malisa (PWANI) na Thobias Mwanakatwe (DAR)

ISHO

Habari Kubwa