Ni zaidi ya sensa

15Sep 2021
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Ni zaidi ya sensa

NI zaidi ya sensa! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mambo yatayoangaziwa wakati wa Sensa ya Sita ya Watu na Makazi nchini inayotarajiwa kufanyika Agosti mwakani.

Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuzindua mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma jana. PICHA: IBRAHIM JOSEPH

Sensa hiyo mbali na kulenga kuiwezesha serikali kutambua idadi ya wananchi wake, itamulika hali ya makazi yao, kama wameajiriwa au hawana ajira pamoja na kujua hali zao kiuchumi.

Rais Samia Suluhu Hassan jana alizindua mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa hiyo, akiitaka Kamati ya Taifa ya Sensa kuwekeza nguvu katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa.

Akizindua mkakati huo jijini Dodoma jana, Rais Samia alisema Sensa ya Watu na Makazi ndiyo itakayowezesha nchi kupata takwimu sahihi zitakazoiongoza serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi wake.

Rais alisema ili sensa ijayo ifanikiwe, Kamati ya Taifa ya Sensa inatakiwa kuweka mikakati ya kutosha kufikisha elimu kwa wananchi.

"Lazima kamati mtumie nafasi yenu kufikisha elimu kwa wananchi ili tuweze kupata takwimu sahihi zitakazotusaidia sisi serikali kufikisha huduma muhimu kwa wananchi wetu wote," alisema.

Rais Samia alisema kufanyika kwa sensa kutawezesha serikali kutambua idadi ya wananchi wake, hali ya makazi yao, kama wameajiriwa au hawana ajira pamoja na kujua hali zao kiuchumi.

"Tukipata takwimu sahihi tutaweza kufikisha huduma kulingana na mahitaji ya watu, hivyo basi lazima elimu itolewe ili kila mtu ahesabiwe bila kumwacha hata mmoja wetu nyuma," aliagiza.

Rais pia aliwataka viongozi wa serikali, vyama vya siasa na wa dini kutumia nafasi zao kuhamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa wakati utakapofika.

“Niwaombe sana viongozi wangu wa dini kutumia nyumba zao za ibada kutoa elimu kwa wananchi ili watambue umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti 2022.

“Sensa zilizokwisha kufanyika nchini ni tano hii ni ya sita na zote zilizopita pamoja na kuitwa za watu na makazi, hakuwahi kuhesabu makazi na kubainisha hali yake, lakini hii tunakwenda kuhesabu kila nyumba na kubainisha hali yake," alisema.

Mkuu wa Nchi huyo alisema kupatikana kwa takwimu za makazi kutaisaidia serikali kupata idadi sahihi na hali yake ili kuiwezesha kuangalia upya Sera ya Makazi Mijini na Vijijini.

"Hivi sasa tumeweka tozo ya pango la ardhi, lakini tulikuwa hatuna takwimu za idadi ya makazi nchini. Zoezi hili pia litatupa anuani za makazi hata kama mtu akikopa mkopo tutajua anatoka wapi na tunampataje," alisema.

Vilevile, Rais alisema takwimu zitakazopatikana wakati wa sensa zitabainisha aina ya nyumba kama ni ghorofa ni ghorofa ngapi na aina gani ya nyumba.

“Ninataka sensa hii ifanyike kwa haraka kwa ufanisi na kwa gharama nafuu," Rais Samia aliagiza.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022, alisema watahakikisha inafanyika kwa ufanisi na kila mtu atayelala nchini usiku wa sensa lazima atahesabiwa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema lengo la Sensa ya Watu na Makazi ni kupata takwimu sahihi zitakazotumika na serikali kutatua kero mbalimbli kwa wananchi wake, hivyo halitakuwa jambo jema kama kuna watu watakwepa kuhesabiwa.

Alisema kupata takwimu ya watu kunaliwezesha taifa kuitumia nguvukazi iliyopo kujenga na kuimarisha uchumi huku kukiwa na mgawanyo sawa wa rasilimali zilizopo.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, alisema Sensa ya Watu na Makazi inakwenda kufanyika kipee kulinganisha na zile zilizopita.

“Sensa hii tunakwenda kutumia mfumo wa TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), hakutakuwa na karatasi kama zile zilizopita, tutatumia vishikwambi ambavyo vitawezesha kupatikana kwa matokeo ya takwimu kwa muda mfupi tofauti na ile ya karatasi ambayo majibu tulikuwa tunayapata baada ya miezi mitatu," alifafanua.

Sensa ya kwanza ya watu na makazi nchini ilifanyika mwaka 1967 kukiwa na wakazi milioni 12.313, ikifuatwa na sensa ya 1978 ambayo ilibaini Tanzania ilikuwa na wakazi milioni 17.513.

 

SENSA TANZANIA

Mwaka    Idadi ya watu     Tanzania Bara   Zanzibar

1967        12,313,469        11,958,654        354,815

1978        17,512,610        17,512,610        476,111

1988        23,095,878        22,455,193        640,685

2002        34,569,232        33,584,607        984,625

2012        44,928,923        43,625,354        1,303,569

Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)

Habari Kubwa