NIDA kuanza kutoza fedha taasisi zinazotumia taarifa zake

13Jul 2020
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
NIDA kuanza kutoza fedha taasisi zinazotumia taarifa zake

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imesema kuwa kuanzia mwezi huu wataanza kutoza fedha taasisi zote za umma na binafsi ambazo zinatumia taarifa za mamlaka hiyo kuhudumia wananchi.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Geofrey Tengeneza katikati akifuatilia kwa makini maelezo ya jinsi “Scaning” ya fomu za Maombi ya Utambulisho wa Taifa inavyofanyika kutoka kwa Afisa Msajili Msaidizi, Nadia Abuu wa ofisi ya Usajili ya NIDA Wilaya ya Ilala.picha na NIDA.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Geofrey   Tengeneza wakati akizungumza na The Guardian Digital.

“Kuna wadau ambao wanatumia taarifa zetu kutoa huduma kwa wananchi napenda niwajulishe kuwa kuanzia mwezi huu (Julai, 2020) tunaanza kutoza tozo kwa taasisi zote za umma na binafsi ambazo zinatumia taarifa zetu kuhudumia wananchi mbalimbali”amesema Tengeneza na kuongeza kuwa;

“Kwa mfano makampuni ya simu, NSSF, Bima ya Afya, mabenki na wadau wengine mbalimbali ambao hili waweze kutoa huduma kwa wateja wao wanahitaji kupata taarifa kutoka kwetu ni lazima kuzilipia ili kuendelea kutoa huduma hiyo”amesema

Ameongeza kuwa taasisi hizo zinapaswa kuingia mkataba na NIDA ili kuweza kupata huduma hizo vinginevyo taasisi ambazo zitashindwa kutimiza matakwa hayo watasitisha huduma hiyo mara moja.

Ameongeza kuwa tayari wametoa notisi kwa kampuni ambazo azijaingia mkataba na NIDA kufanya hivyo mpaka Julai 31, 2020 na kwa ambazo zitashindwa watasitisha huduma.

“Kampuni 17 tayari tumewatumia notisi kuanzia Agosti Mosi kama watakuwa hawajaleta maombi kwetu ili kuwapatia mkataba tutawakatia huduma pia tunaendelea kufanya upembuzi kujua ni makampuni gani wanatumia huduma zetu,”amesema 

Amesema kuwa kwa hatua ya awali wanategemea kuingia mkataba na watumia taarifa za NIDA zaidi makampuni na taasisi 86.

Amesema kuwa utaratibu huo ni maelekezo kutoka kwa Serikali yalioelekeza NIDA kuanza kujitegemea kukusanya fedha kutumia utaratibu huo ili kuondokana na utaratibu wa kupata fedha za matumizi kutoka serikalini.

 “Mpaka sasa kampuni 65 zimeleta maombi ya kusaini mkataba na pia tumepeleka mikataba kwa kampuni 36 bado hawajarudisha, pia makampuni 18 wamerudisha mikataba na 12 kati yao tayari tushasaini nao mkataba”amesema

Habari Kubwa