Njia kuu kuongeza fedha mitaani hii

03Aug 2017
Romana Mallya
Dar es salaam
Nipashe
Njia kuu kuongeza fedha mitaani hii

TAASISI ya sekta binafsi Tanzania (TPSF), imesema njia pekee ya kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi ni serikali kurejesha fedha kataika benki za biashara.

Hali hiyo inatokana na utafiti uliofanywa na TPSF, kuhusu serikali kuondoa fedha zake kwenye benki za biashara, umebaini kuwapo kwa mzunguko mdogo wa uwekaji fedha kwenye benki na kuongezeka kwa riba ya mikopo.

Mwaka jana, Serikali iliondoa fedha zake kwenye benki za biashara na kuziweka kwenye akaunti ya pamoja iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uhamasishaji, Sera na Utafiti wa TPSF, Gili Teri, alisema wamebaini hatua hiyo imesababisha kupungua kwa amana kwenye benki na wafanyabiashara wa sekta binafsi kutokopesheka.

Alisema athari hizo zinasababishwa na kupungua uwekaji wa fedha kwenye benki hizo. “Tunapozungumzia uchumi wa viwanda ni pamoja na wafanyabiashara kutoka sekta binafsi, hivyo lazima taasisi za fedha ziwe na uwezo wa kuwakopesha watu hawa ili viwanda vijengwe,” alisema.

Teri alisema utafiti umebaini mfumo huo wa kupeleka fedha BoT umeinufaisha serikali na kuiwezesha kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ukiwamo ujengwaji wa barabara na reli.

Kuhusu mapendekezo, Teri alisema kutokana na utafiti kubaini Watanzania wengi hawana akaunti za benki, benki za biashara nchini zinapaswa kufanya kazi ya ziada ili kupata akiba kutoka kwa watu ambao hawatumii huduma za kibenki ili kuziba pengo lililoachwa na serikali la kutoa fedha zake.

Pia walipendekeza BoT isaidie mamlaka ya Serikali za Mitaa kuanzisha, kupitia na kutekeleza hatua thabiti na mifumo kwa ajili ya kutumia akaunti hiyo ya Hazina kuongeza makusanyo ya mapato ya serikali na usambazaji wa fedha za serikali.

Alisema serikali inapaswa kushirikisha matokeo ya utekelezaji wa sera mbalimbali za serikali kama njia ya kutathmini mafanikio ya uamuzi uliofanywa na serikali wa kuondoa fedha kwenye benki za biashara na kuzihamishia kwenye akaunti moja iliyoko BoT.

Alisema serikali inapaswa kuwafahamisha wadau wote na umma kwa ujumla manufaa ya akaunti moja iliyoko BoT katika suala zima la kuleta maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Aidha, alisema mapendekezo ya utafiti huo yaliyowasilishwa jana mbele ya wadau, yatawasilishwa serikalini ili hatua zikuchukuliwe.

Habari Kubwa