Njozi yatimia serikali kuhamia Dodoma

21May 2023
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe Jumapili
Njozi yatimia serikali kuhamia Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema uzinduzi wa jengo jipya la Ikulu ya Chamwino ni uthibitisho wa kukamilika kwa adhma ya serikali ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu, kwamba hakuna kurudi nyuma.

Aliyasema hayo jana Chamwino mkoani hapa wakati akizindua jengo hilo katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwamo marais wastaafu wa awamu zilizopita.

“Wale waliokuwa na mashaka ya kutimia kwa shughuli ya kuhamia Dodoma kwa sasa wameamini hakuna kurudi nyuma ‘We are here to stay’, tupo Dodoma, Dar es salaam tutakwenda kupokea wageni wetu wa kimataifa, tutakwenda kufanya kazi zinazopaswa kufanywa Dar es Salaam.

“Tutakapomaliza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato na nyumba zetu katika awamu ya pili ya ujenzi wa Dodoma hata wageni wa kimataifa tutawapokea hapa hapa Dar es Salaam tunaiacha kuwa mji wa biashara,” alisema.

Rais Samia alisema Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na Hayati John Magufuli ilitekeleza azma ya serikali kuhamia Dodoma kwa msukumo zaidi.

“Julai 2016 Hayati Magufuli alikumbusha mkutano mkuu wa CCM kuhusu uamuzi wa kuhamisha shughuli za serikali kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma na siku mbili baadaye Siku ya Mashujaa, alisisitiza dhamira yake na baada ya hapo, utekelezaji wa miradi mbalimbali Jiji la Dodoma uliendelea kwa kasi zaidi ikiwa ni pamoja na upanuzi wa Ikulu ya Chamwino.

“Mzee wetu Mwinyi alisema maisha ni hadithi na kututaka tujitahidi kuandika hadithi njema za maisha yetu. Katika utekelezaji wa wazo hili la kuhamishia serikali Dodoma. Hakika Hayati Magufuli ameandika hadithi yake hatutaweza kuandika historia ya shughuli hii bila kuwepo kwa tahariri ya mchango wake mkubwa,” alisema.

Samia alisema mchakato wa kuhamishia serikali mkoani Dodoma ulikuwa wa muda mrefu na wa kidemokrasia na ujenzi huo ni wa nguvu za awamu zote za uongozi.

Alisema alipokabidhiwa uongozi aliahidi kuendeleza mema yaliyopo, kuboresha na kuleta mema mapya kwa misingi ya kauli mbiu ya kazi iendelee.

“Ujenzi wa Ikulu ni moja ya miradi niliyorithi kutoka kwa Hayati John Magufuli, mtakumbuka mradi wa kwanza kukamilisha ulikuwa Daraja la Tanzanite huu ni mradi wa pili na inshallah Mungu anipe uwezo niikamilishe yote,” alisema.

SAMIA COMPLEX NDANI YA IKULU

Rais alisema katika eneo la Ikulu bado kuna kazi za kufanya na hatua inayofuata ni ujenzi wa jengo la kisasa ambalo litaitwa ‘Samia Complex’ litakalokuwa na ukumbi wa mikutano utakaochukua watu 2,000 hadi 3,000, nyumba za viongozi hasa wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

 “Kutakuwa na Zanzibar Lounge, East Africa Lounge, kutakuwa na uwanja wa gofu, njia ya ndege, viwanja vya michezo mbalimbali, sehemu za historia za viongozi wa nchi yetu, michoro ipo tayari tunahangaika kutafuta fedha ili kuanza ujenzi huo,” alisema.

HISTORIA MAKAO MAKUU

Rais Samia alisema mwaka 1966 Mbunge wa Musoma, Joseph Nyerere, ambaye alikuwa mdogo wa Hayati Mwalimu Nyerere, aliwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka makao makuu ya serikali yahamishiwe Dodoma jambo ambalo lilipingwa, hoja yake kuondolewa.

“Aprili 1972 Kamati ya Utendaji ya TANU ya Mkoa wa Mwanza iliibua tena wazo hili na kuliwasilisha pendekezo rasmi kwa Kamati Kuu ya TANU na kuamua pendekezo hilo lijadiliwe kwenye matawi yote 1,859 ya TANU yaliyokuwepo wakati huo na kufanyiwa uamuzi na matokeo yake matawi 1,017 yaliunga mkono na matawi 842 yalipinga,” alisema Rais Samia.

Ilipofika mwaka 1973, alisema Halmashauri Kuu ya TANU ilipitisha azimio kwamba makao makuu ya serikali yahamishiwe Dodoma na kazi hiyo ifanyike katika kipindi cha miaka 10.

“Tangu mwaka 1973 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,  alivyoutangazia umma kazi ya kuendeleza mji ilianza na haikuwa rahisi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo za kiuchumi na kuifanya safari hiyo kuwa ndefu zaidi kuliko ilivyopangwa,” alisema Rais Samia.

Alisema safari hiyo ilikuwa ndefu kuanzia mwaka 1973 hadi 2023 na imekuwa ya miaka 50 badala ya miaka 10 iliyoagizwa na Halmashauri Kuu ya TANU.

MAELEKEZO YA SERIKALI

Akitoa maelezo mafupi ya serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Moses Kusiluka, alisema uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo ulifanyika Mei 30, 2020 na uliongozwa na Hayati Rais John Magufuli ambaye aliambatana na marais wastaafu.

Alisema Ikulu ya Dar es Salaam ilijengwa na wakoloni na ujenzi wake ulikamilika mwaka 1923, kwamba ni miaka 100 imepita tangu ijengwe.

“Mradi umetekelezwa na Watanzania kwa asilimia 100, ujenzi umefanywa na Jeshi la Kujenga Taifa na Wakala wa Majengo Tanzania alikuwa mshauri elekezi na Ofisi ya Rais nayo ilisimamia kwa karibu sana.

“Ujenzi wa barabara ulisimamiwa na Wakala wa Barabara nchini kwa kiasi kikubwa vifaa vya ujenzi vimezalishwa hapa nchini na samani za jengo hili zimetengenezwa nchini,”alisema.

Alisema kukamilika kwa jengo hilo kunatimiza adhma ya serikali kuhamia Dodoma na Rais Samia alipoingia madarakani ujenzi wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 70.

MIAKA MIWILI YA SAMIA

Katibu Mkuu huyo alisema katika ujenzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za serikali kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 70 na utekelezaji wake unatarajia kugharimu zaidi ya Sh.bilioni 700.

“Mradi mwingine ni ujenzi wa makao makuu ya Mahakama ambao umekamilika kwa asilimia 91 na gharama yake ni Sh.bilioni 129.7,”alisema.

Kadhalika, alisema miradi mingine mikubwa ambayo ilianza na kuendelezwa katika uongozi wake ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao umegharimu Sh. bilioni 360, ujenzi wa barabara ya mzunguko yenye urefu wa kilometa 112.5 jijini Dodoma ambao gharama yake ni Sh.bilioni 221.7.

Alisema serikali imeendelea na ujenzi wa miradi mingi ikiwamo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao Rais Samia alipoingia madarakani ulikuwa umeanza kwa vipande viwili vyenye kilometa 722 ambavyo ni Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora.

Alibainisha kuwa ujenzi wa vipande hivyo vyote vinagharimu Sh.trilioni 23.3 na hadi sasa Sh.trilioni 8 zimetumika.

“Mradi wa kufua umeme wa maji wa bwawa la Mwalimu Nyerere Rais Samia alipoingia madarakani ulikuwa umefikia asilimia 31.6, hadi sasa umefikia asilimia 86.8 na utagharimu Sh.trilioni 6.5 na hadi Aprili mwaka huu makandarasi walikuwa wamelipwa Sh.trilioni 5.3,” alisema.

Pia alisema kwa miaka miwili iliyopita serikali ilikamilisha ujenzi wa barabara kuu zenye urefu wa kilometa 471.5 na bado kazi inaendelea na unagharimu Sh.trilioni 2.5.

Hivyo alimhakikishia Rais Samia kuwa majengo hayo yatatunzwa na kusimamiwa vizuri na eneo la Ikulu litakuwa mfano bora wa utunzaji wa mazingira na kuthibitisha kuwa Dodoma ya kijani inawezekana.

HALI ILIVYOKUWA

Katika sherehe hizo Rais Samia aliwasili majira ya saa 4:15 asubuhi kwenye mzunguko wa tembo na kupokelewa na kushangiliwa na wahamasishaji na baadaye kupita mbele ya gadi ya heshima na pia kukagua gwaride maalum.

Ili kuweka kumbukumbu, Rais Samia alipanda mti wa uzinduzi na kufuatiwa na kufungua jiwe la ufunguzi wa jengo akishirikiana na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Pamoja na hayo, Rais Samia na viongozi wengine walishuhudia gwaride maalum la upandishaji bendera, alipiga ngoma maalum, alikagua jengo na kukata utepe wa kufungua jengo hilo.

Katika sherehe hizo, tuzo maalum za Rais zilitolewa kwa Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Magufuli kwa kutambua mchango wao wa kuhamishia serikali Dodoma.