NMB Teleza Kidijitali yazinduliwa mtaa kwa mtaa D’Salaam

10May 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
NMB Teleza Kidijitali yazinduliwa mtaa kwa mtaa D’Salaam

BENKI ya NMB imezinduwa rasmi Kampeni ya Teleza Kidijitali, ambayo imelenga kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa kutumia na kunufaika na huduma zilizo chini ya kampeni hiyo za NMB Pesa Wakala, Lipa Mkononi na Mshiko Fasta.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akizungumza na mfanyabiashara wa vitambaa, Juma Hamad (kulia), walipokuwa wakitembea mitaani kuinadi Kampeni ya Teleza Kidijitali kwa Mkoa wa Dar es Salaam, iliyofanyika Tawi la Benki ya NMB Tandika jana. Katika kampeni hiyo wafanyakazi wa NMB walitembea mitaani na kutoa elimu kwa wateja kuhusu mikopo ya Mshiko Fasta, Lipa Namba na NMB Pesa Wakala na kufungua akaunti. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kampeni ya Teleza Kidijitali ilizinduliwa Aprili 11 mwaka huu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, jijini Dodoma.

Timu ya NMB ikiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna imeipelekea kampeni hiyo mtaani kuwaelimisha wateja na wasiokuwa wateja umuhimu wa huduma zilizo chini ya mwamvuli huo, ambazo ni NMB Pesa Wakala, Lipa Namba na Mshiko Fasta.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika katika Tawi la NMB Tandika wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, ambako pia Zaipuna, aliambatana na Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, kuzindua na kisha kuwatembelea wafanyabiashara madukani ili kuwapa elimu zaidi. 

 Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Zaipuna alisema ujio wake yeye na viongozi wengine waandamizi wa NMB Makao Makuu na kuungana na wale wa Tawi la Tandika, umelenga kutoa elimu ya kutosha na kuwaingiza Watanzania wengi zaidi kwenye Sekta Rasmi ya Kifedha ili waweze kunufaika na huduma mbalimbali ambazo wanazitoa.

 “Tuko hapa kunadi huduma zote muhimu zilizo kwenye mwamvuli wa Teleza Kidijitali, ambazo ni Mshiko Fasta ambayo ni mikopo nafuu isiyo na dhamana, inayopatikana kwa njia ya simu kwa wateja wenye akaunti, ambako mteja hatahitaji kitambulisho wala dhamana yoyote kuupata.

 “Pia tumeutumia uzinduzi wa kampeni hii kwa ujumla kunadi huduma ya Lipa Mkononi, ambayo itamwezesha mfanyabiashara kuitumia kulipwa na wateja wake kwa kutumia namba ya malipo au kuskani QR, huku ikitupa sisi kumbukumbu na historia ya mfanyabiashara ambayo itasaidia hata katika utoaji wa mikopo. 

 “Pia tumekuja na NMB Pesa Wakala, huduma inayomwezesha mtu yeyote kuwa wakala bila kutumia mashine, ambayo itamwezesha kutoa huduma za kuweka, kutoa ama kutuma pesa kirahisi kwa kutumia hata simu ya kitochi,” alisema Zaipuna, ambaye alishiriki kutembelea wafanyabiashara wa eneo la Tandika madukani mwao kutoa elimu na kusikiliza maoni yao.

 Zaipuna aliielezea kampeni hiyo kwamba imelenga kuhakikisha wanawapa elimu Watanzania waweze kuwa sehemu ya watumiaji wa huduma za sekta rasmi ya kifedha na kwamba wanaamini NMB Pesa Wakala, Lipa Namba na Mshiko Fasta, vitakuwa chachu ya ukuaji kibiashara na kiuchumi kwa wateja wao kote nchini, ambako wameahidi kuifikisha  Teleza Kidijitali.

Richard, aliwataka wakazi wa kanda yake kuchangamkia Teleza Kidijitali, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bila kusumbuka kwenda matawini, ili kuokoa muda wa kufanya shughuli nyingine za kukua kiuchumi.

“Wito wangu kwa wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla, inayojumuisha Zanzibar na mkoa wa Pwani, ni vema wanapofikiria kufungua akaunti, wafanye hivyo na Benki ya NMB, ambako watapata manufaa makubwa na masuluhisho mbalimbali huku tukiwa sehemu ya ustawi wao kibiashara na kiuchumi,” alisisitiza Donatus.

Habari Kubwa