NMB yatoa vifaa vya mil. 180/- elimu, afya

18Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
NMB yatoa vifaa vya mil. 180/- elimu, afya

KATIKA kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja Benki ya NMB imetoa vifaa mbalimbali vya ujenzi, na samani kwenye sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari ikiwamo vifaa vya afya katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Simiyu, Iringa, Rukwa, Mara, pamoja na Kilimanjaro.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (watatu kulia), akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka (wanne kulia), msaada wa mashuka na vitanda kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Wengine kutoka kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mukunda na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Bahi, Keneth Nolo.PICHA: MPIGAPICHA WETU

Katika kuadhimisha wiki hiyo ambayo ilianza Oktoba 3, 2021 ikiwa na kauli mbiu Nguvu ya Huduma (The Power of Service), benki hiyo imetoa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh. milioni 180.25 lengo likiwa kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha sekta ya elimu na afya.

Katika mkoa wa Dodoma, Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alikabidhi viti 200 na meza 200 kwa ajili ya shule za sekondari za Nondwa, Msisi Juu na Bahi za Wilaya ya Bahi na Shule ya Sechelela katika Jiji la Dodoma.

Mtendaji mkuu huyo wa NMB akikabidhi vifaa hivyo kwa mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka, alisisitiza ushirikiano wa benki hiyo na wananchi katika utoaji huduma utaendelea kuimarika nchi nzima.

Zaipuna alikabidhi pia madawati 50 kwa Shule ya Msingi Chiguluka, mabati ya kuezekea Sekondari ya Bahi na vifaa vya hospitali kwa zahanati za Chimendeli na Hospitali ya Wilaya Bahi na kuzindua hati ya kiapo cha huduma kwa wateja ikilenga kutoa nafasi kutoa huduma kwa saa 24.

Mtaka aliomba NMB kuendelea kuangalia na makundi mengine yenye uhitaji hasa wanawake na kwamba wasione shida wanapoombwa misaada kwani kinachowaponza ni ukubwa wao ukilinganisha na benki zingine nchini.

Mkoani Mara NMB imetoa msaada wa madawati 100 yenye thamani ya zaidi ya Sh. 10 milioni kwa Shule ya Msingi Kiriba iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini.

Msaada huo umesaidia kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa madawati, lilokuwa likiikabili shule hiyo kwa muda mrefu na kueplekea baadhi ya wanafunzi kukaa chini wakati wa vipindi.

Mkoani Kilimanjaro benki hiyo imetoa vifaa mbalimbali vya elimu kwenye shule za sekondari wilayani Moshi mkoa humo vyenye thamani ya Sh. milioni 40 ikiwa ni sehemu kurejesha sehemu ya faida kwa wateja wake na kuunga mkono juhudi za serikali kuinua sekta ya elimu nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Said Mtanda, akipokea vifaa hivyo ambavyo ni madawati na vifaa vya kuezekea, alisema mchango wa benki ya NMB wataendelea kuuenzi kwasababu unasaidia kupunguza changamoto za sekta ya elimu.

Shule zilizonufaika na vifaa hivyo ni Shule ya Msingi Mawalla, Shule ya Sekondari Mwika, Shule ya Sekondari Mangoto, Shule ya Sekondari Mieresini na Shule ya Sekondari Himo Sekondari zilizochangiwa mabati 293 na madawati 300 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya masomo kwa wanafunzi.

Mkoani Arusha Benki hiyo imetoa vifaa mabati, madawati, vitanda, viti na meza wa shule mbalimbali kutoka Wilaya za Arusha mjini, Arusha Vijijini, Karatu Meru Vijijini pamoja na Monduli Vijijini vikiwa na thamani ya Sh. milioni 45.

Katika Mkoa wa Simiyu benki hiyo imetoa madawati, meza na viti, mabati pamoja na mbao kwa ajili ya shule nne za msingi na Sekondari katika Wilaya ya Maswa vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 24.

Akikabidhi vifaa hivyo Meneja Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse, alisema kuwa NMB imetoa vifaa hivyo ili kuhakikisha mazingira ya wanafunzi kusomea yanakuwa mazuri ili watoto waweze kufikia malengo yao.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Aswege Kaminyoge, akipokea vifaa hivyo aliishukuru benki hiyo, huku akiwataka walimu na wanafunzi kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa kwa makini ili kuweza kukaa muda mrefu.

Katika Mkoa wa Iringa Benki hiyo imetoa madawati 50 kwa shule ya msingi Itunduru yenye thamani ya Sh. milioni tano, huku Mkoani Rukwa katika shule ya msingi Mfaranyaki ikitoa mabati 200 yenye thamani ya Sh. milioni 6.25.

Morogoro, pia imetoa vifaa vya afya kwa ajili ya hospitali mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vyenye thamani ya Sh. milioni 10.

Habari Kubwa