NMB yawalipa bima ya mil.438/ wafanyabiashara Kariakoo

28Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
NMB yawalipa bima ya mil.438/ wafanyabiashara Kariakoo

BENKI ya NMB kupitia Kampuni ya Reliance Insurance, zimewalipa bima ya Sh. milioni 438.4 wafanyabiashara 12 waliokata bima mbalimbali, kati ya waliounguliwa moto maduka yao katika Soko la Kariakoo, Julai 10, mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya NMB, Martine Massawe akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi kwa wafanyabiashara waliokuwa na Bima waliounguliwa katika Soko Kuu la Kariakoo. Kushoto ni Meneja Madai wa kampuni ya bima ya Reliance, Joel Mwakalebela na kulia ni Meneja wa Bima Benki ya NMB, Adam Nsenga.

Hafla ya kuwakabidhi wafanyabiashara hao hundi yenye thamani hiyo, ilifanyika jana  katika Ofisi za NMB Kariakoo Business Center, ambako waathirika hao walikiri kuwa hasara na maumivu yao ya kuunguliwa yamepozwa na malipo hayo ya haraka ya bima.

Akizungumza kabla ya kuwakabidhi hundi ya mfano, Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya NMB, Martin Massawe, alitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni chanya wa kuzilinda kwa bima mali na pesa wanazotafuta kwa jasho lao ili kuepuka maumivu yasiyo na mfariji wakati wa majanga.

Meneja wa Madai wa Kampuni ya Bima ya Reliance, Joel Mwakalebela akipongezana na mmoja wa wafanyabiashara waliounguliwa na Moto katika Soko Kuu la Kariakoo, Emmanuel Kabadi (kushoto) baada ya Benki ya NMB kukabidhi mfano wa hundi ya zaidi ya Shilingi Milioni  438 kwa wafanyabiashara 12  waliokuwa na Bima. Kushuto ni Sajida Kagasheki  mmoja wa wafanyabiashara na Kulia ni Meneja wa Bima wa Benki ya NMB, Adam Nsenga.

“Tuko hapa kwa ajili ya kuwafuta machozi wafanyabiashara waliokata bima nasi kupitia mikopo yao ama waliokuwa na bima za mali bila mikopo, ambao walikuwa sehemu ya wahanga wa moto wa Julai 10, sokoni Kariakoo.

“Wito kwa Watanzania, moto wa Soko la Kariakoo uwe fundisho kwao juu ya umuhimu wa bima. Moto ama majanga huja bila kuyatarajia, unapokata bima unakuwa umejiwekea kinga kuilinda pesa ama mali uliyotafuta kwa jasho lako.

“Uwapo wa bima hukurejeshea nguvu haraka kana kwamba hakuna janga lililokutokea. Wito huu sio tu kwa bima za mikopo, bali mali zote kwani gharama za bima hizi ni nafuu mno,” alisema Massawe mbele ya waathirika hao 12, ambao ni miongoni mwa waathirika wa moto sokoni Kariakoo.

 Mkuu wa Kitengo cha Bima wa Benki ya NMB, Martine Massawe (katikati) akikabidhi mfano wa hundi  ya Sh. Milioni 438 kwa wafanyabiashara 12 waliokuwa na Bima waliounguliwa katika Soko la Kuu la Kariakoo, Sajida Kagasheki na Emmanuel Kabadi (kushoto) wakati wa makabidhiano yaliyofanyika katika katika Tawi la NMB Kariakoo Business Center. Kutoka kulia ni Meneja wa Bima wa Benki ya NMB, Adam Nsenga na Meneja wa Kampuni ya Reliance, Joel Mwakalebela.

Akisisitiza umuhimu na unafuu wa bima hizo, Massawe alitolea mfano wa bima ya moto kuwa hukatwa asilimia 0.25 ya thamani ya mali na kwamba kama mali ya Sh. milioni 100, makato yake ya bima ni Sh. 150,000 tu bila V.A.T kiasi ambacho ni rahisi kuliko bima za magari.

“Nyumba ya thamani ya Sh. Mil. 100, makato yake ya bima ni Sh. 150,000, sawa na 177,000 pamoja na V.A.T, hapa utaona ni kwa namna gani bima hizi ni nafuu, lakini zinazobeba nguvu kubwa majanga yanapotokea,” alisema Massawe, na kuongeza kuwa moto ulipotokea walikuwa wa kwanza kukimbilia ili kujua hasara za wateja wao.

Joel Mwakalebela, Meneja Madai wa Kampuni ya Reliance Insurance, aliwapongeza waathirika hao kwa uamuzi wao wa kukata bima, huku akisisitiza Watanzania kutosubiri mikopo ili kukata bima, badala yake watumie huduma hizo ili kujilinda na majanga.

“Tukio la moto Kariakoo litufundishe kuwa bima sio tu ni kwa ajili ya pesa za mikopo, nenda kakate bima za moto, magari, nyumba, afya, mali na nyinginezo, kwa sababu majanga hayaepukiki, na pia yanapokuja hayapigi hodi kwetu.”

Emmanuel Mbise, mmiliki wa maduka namba 019 na 026 yaliyoteketea kwa moto, alifichua kuwa maumivu waliyoyapata waathirika wa tukio hilo ni makubwa, lakini malipo ya bima kutoka NMB, yanawapa hafueni na faraja kubwa.

Naye Sajida Kagasheki, alisema amepata faraja kubwa kupitia malipo hayo ya bima, huku akiwataka Watanzania kukimbilia sana huduma za bima, ambazo ni mkombozi na mfariji wa kweli wakati wa matatizo kama ya moto, vifo, ulemavu, upotevu na kadhalika.