Norway yamwaga mabilioni tena kuimarisha biashara

07Dec 2017
Christina Mwakangale
Nipashe
Norway yamwaga mabilioni tena kuimarisha biashara

NORWAY imetoa Sh. bilioni 13.4 kwa taasisi ya TradeMark East Africa (TMEA) kwa ajili ya kuimarisha biashara za Watanzania kwenye mipaka ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Balozi wa Norway nchini, Hanne-Marie Kaarstad, aliwekeana saini ya makabidhiano ya fedha na Mwenyekiti wa Bodi ya TMEA, Ali Mufuruki, jijini Dar es Salaam.

Taasisi hiyo inazijengea uwezo bidhaa za Tanzania ili zikidhi viwango vya ubora, kuhimili ushindani na kuingia kwenye masoko ya nchi za EAC, Afrika na masoko ya kimataifa.

Balozi wa Norway nchini, Hanne-Marie Kaarstad, aliwekeana saini ya makabidhiano ya fedha hizo jana na Mwenyekiti wa Bodi ya TMEA, Ali Mufuruki, jijini Dar es Salaam.

Kaarstad alisema Norway imeshuhudia taasisi hiyo ikijitahidi kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa nchi sita wanachama na kuweka mazingira rafiki ya kibiashara.

“Tangu kuanza kwa taasisi hii mwaka 2011 imekuwa ikihakikisha inaweka mazingira mazuri ya kibiashara katika maeneo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Shirika la viwango Tanzania (TBS) kuongeza ufanisi kwa asilimia 50,” alisema Kaarstad.

Mufuruki alisema fedha zitaongeza ufanisi hususan kwa vikundi vya kiabiashara vya kinamama kwa kuweka miundombinu bora ili kupunguza vikwazo vya biashara.

Alisema taasisi hiyo imefanikiwa kupunguza muda uliokuwa unatumika kwa wafanyabiashara wa zaidi ya saa 48 hadi saa mbili kwa sasa, ili kukamilisha taratibu za kibiashara mpakani.

“Hivi sasa muda wanaotumia wafanyabiashara ni chini ya saa mbili ili kupita mipaka ya Holili, Mutukula na Kabanga. Hii imesaidia hasa kinamama ambao ni wafanyabiashara zaidi kwenye mipaka ya EAC,” alisema Mufuruki. 

Habari Kubwa