NSSF, PSPF, zajitosa uwekezaji viwanda 27

27Oct 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
NSSF, PSPF, zajitosa uwekezaji viwanda 27

MIFUKO ya hifadhi ya jamii nane imeanza utekelezaji wa mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuwekeza kwenye viwanda kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kujenga na kufufua viwanda 27 nchini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mifuko ya Hifadhi Tanzania (TSSA), Meshack Bandawe.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mifuko ya Hifadhi Tanzania (TSSA), Meshack Bandawe, alisema hivi karibuni katika mkutano wa wadau wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa wanashirikiana na wizara tano kutekeleza mpango huo. Baadhi ya mifuko iliyogeukia uwekezaji huo ni NSSF, PSPF, LAPF, WCF, NHIF, GEPF na PPF.

Alisema miradi hiyo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji lengo likiwa ni kufikia asilimia 40 ya ajira zinazotokana na sekta ya viwanda nchini na ajira zisizo rasmi kutokana na kuwapo kwa mnyororo mrefu wa thamani.

Bandawe alitaja miradi kwa kila mfuko kuwa ni NSSF ambao wametoa mkopo wa zaidi ya Sh. bilioni 4 kwa kiwanda cha Viuadudu Kibaha mkoani Pwani, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo (NDC).

Mwingine ni kufufua vinu vya usagaji wa nafaka vya NMC Iringa, Dodoma na Arusha ambavyo vitapewa mikopo; ufufuaji wa kiwanda cha matairi Arusha (General Tyre) na uwekezaji wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari Mkulazi mkoani Morogoro, kwa kushirikiana na Mfuko wa Pensheni (PPF).

Aliitaja miradi ya PPF ni ujenzi wa jengo la uzalishaji kwa ajili ya kampuni ya Tooku Garments katika eneo la BWM SEZ - Dar es Salaam na upanuzi wa kiwanda cha viatu cha Magereza Karanga mkoani Kilimanjaro, kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza.

Mfuko wa PSPF utashiriki katika miradi ya ujenzi wa eneo maalumu la kiuchumi (SEZ) katika eneo la Kurasini Logistic Center, Dar es Salaam na ujenzi wa kiwanda cha Agave Syrup kinachotumia malighafi itokanayo na mabaki ya mkonge mkoani Tanga.

Bandawe alitaja mfuko mwingine kuwa ni LAPF, ambao utafufua kiwanda cha chai cha Mponde, Lushoto mkoani Tanga na mradi wa kutengeneza bidhaa za hospitali.
Mfuko wa GEPF utafanya mradi wa ujenzi na ufufuaji wa ‘foundary’ kwa ajili ya vipuri katika kiwanda cha Machine Tools mkoani Kilimanjaro, ujenzi wa machinjio ya kisasa kwa kushirikiana na Ranchi ya Taifa (Narco) na Benki ya Uwekezaji (TIB) mkoani Pwani.
Mingine ni kiwanda cha kusindika juisi na mvinyo utokanao na zabibu Chamwino mkoani Dodoma, ufufuaji na uendelezaji wa kiwanda cha kubangua korosho Tandahimba na Newala mkoani Mtwara kwa kushirikiana na TIB.

Bandawe alisema TSSA itakuwa na miradi ya pamoja ambayo ni ufufuaji, uendelezaji au uanzishwaji wa viwanda vipya vya sekta ya ngozi na bidhaa za ngozi, na viwanda vipya vya uchongaji wa vipuri.

“Ili kurahisisha utekelezaji wa ujenzi wa viwanda nchini baadhi ya mifuko itashirikiana na Suma JKT katika utekelezaji wake,” alibainisha.

Katibu Mkuu huyo alisema mifuko ambayo inaendelea na majadiliano kwa nia ya kuanza utekelezaji wa uendelezaji wa viwanda ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) utakaojihusisha katika kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu.

Alibainisha kuwa kwa kuanzia, mfuko huo umepanga kuanza uzalishaji wa dawa na bidhaa hospitalini, uzalishaji wa maji tiba na uzalishaji wa gesi kwa ajili ya tiba.

“Mapitio ya awali ya mfuko wa NHIF yameonesha fursa za uwekezaji katika maeneo ya kufufua viwanda vilivyopo katika hospitali mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza bidhaa za hospitali kwa ubia na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kiwanda cha kuzalisha gesi ya oksijeni katika Taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI),” alibainisha na kuongeza:

“Kuanzisha kiwanda cha kutengeneza dawa kali kwa ubia na Bohari Kuu ya dawa (MSD) na kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kufufua uzalishaji wa dawa katika kiwanda cha dawa kinachomilikiwa na jeshi hilo Mgulani, kwa kujenga kiwanda kikubwa cha kisasa cha kuzalisha dawa na bidhaa mbalimbali za hospitali katika kambi ya Ruvu.”

Bandawe alisema mfuko wa ZSSF utaingia katika uvuvi Bahari Kuu na usindikaji wa samaki na kwamba kwa pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), watashirikiana katika miradi ya pamoja ya TSSA.

Aidha, alisema wanaendelea kufanya utafiti wa maeneo ya uwekezaji katika viwanda vya nguo, bidhaa za ngozi na utengenezaji wa vipuri na baada ya utafiti, maamuzi ya pamoja ya eneo gani iwekeze yatatolewa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka, alisema mifuko inaweza kuwekeza kwenye viwanda kwa kufuata misingi ya uwekezaji ili kulinda maslahi ya wanachama wao.

“Mwongozo wa uwekezaji unatoa fursa kwa mifuko kuwekeza kwenye viwanda kwa mifumo mbalimbali, kushiriki uwekezaji popote kwenye mzunguko wa uwekezaji na mpango wa fedha.

Inaweza kuwekeza kwa mikopo, hati fungani, majengo huku wakiangalia upatikanaji wa huduma za usafiri, mawasiliano, nishati endelevu na miundombinu ya kijamii,” alifafanua.

Aidha, alitolea mfano wa uwekezaji wa mifuko nchini Afrika Kusini, akiutaja Mfuko wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali nchini humo ambao mwaka huu umewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 158 (zaidi ya na Sh. trilioni 346).

Habari Kubwa