NSSF yaachana na mashangingi

11Apr 2017
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
NSSF yaachana na mashangingi

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeamua kuacha kununua magari ya kifahari yenye injini kubwa, maarufu kama mashangingi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kubana matumizi yake kwa asilimia 30 kuanzia mwaka jana.

Lengo la NSSF katika kubana matumizi, imeelezwa, ni kuelekeza kwenye uwekezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo viwanda, fedha zitakazookolewa.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema maboresho ya uendeshaji, hayo yamefanyika katika kipindi cha mwaka mmoja na kwamba mkakati mkuu ni kupunguza zaidi matumizi.

Katika ubanaji huo wa matumizi, NSSF imeacha kununua magari ya kifahari na badala yake itakuwa na ya kawaida lakini yatakayowezesha utendaji kazi kwenye ofisi zote nchini.

Prof Kahyarara alisema kiasi cha fedha ambacho kimeokolewa kutokana na mkakati huo wa kubana matumizi kimeelekezwa kwenye uwekezaji wa viwanda ambavyo vitawezesha zaidi ya Watanzania 100,000 kuajiriwa.

Viwanda vinavyojengwa na NSSF kwa ushirikiano na wadau wengine ni Mkulazi na Mbigili mkoani Morogoro ambavyo ni vya sukari.

Mfuko huo pia umetoa mikopo kwa viwanda vya usagishaji vya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko vya Iringa na Dodoma na cha viuadudu mkoani Pwani.

Akizungumzia maendeleo, Prof Kahyarara alisema matumizi ya shirika, ikiwamo kulipa mafao na gharama za uendeshaji kwa sasa ni asilimia 31 ya makusanyo.

“Hatua hii inalifanya shirika kubaki na uwezo mkubwa wa kugharamia miradi inayoendelea kutekelezwa na kubuni miradi mipya ya uwekezaji ikiwamo viwanda,” alisisitiza.

Alisema NSSF imeweka mikakati kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa ujenzi wa uchumi wa viwanda bila kuathiri majukumu yake mengine ya msingi.

Kwa mujibu wa Prof Kahyarara, shirika limeongeza makusanyo kwa asilimia 30 kuanzia Julai mwaka jana hadi sasa.

“Shirika limepunguza sana matumizi katika maeneo makubwa mawili, kwanza matumizi ya kawaida ambayo yamepungua kwa asilimia 30 na tutapunguza zaidi, (na) pili kuwa makini katika matumizi na uhakiki wa matumizi yote,” alisema.

Alisema jitihada hizo zimesaidia kupunguza matumzi katika malipo ya mafao kwa asilimia 70.

Aidha, alisema NSSF imeokoa fedha kwa kuongeza udhibiti katika malipo ambao umeondoa kwa kiasi kikubwa madai yatokanayo na kughushi nyaraka mbalimbali kwa lengo la kujipatia fedha ndani ya shirika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, wamebaini na kukamata nyaraka za maombi feki 1,600 na mawakala 12 ambao walikuwa wanasaidiana na wanachama wa mfuko huo kughushi nyaraka za shirika ili kujipatia fedha.

Alisema kesi 10 zimefunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini na wafanyakazi wa NSSF 32 wamefukuzwa kwa makosa ya kughushi, kujaribu kuiba na wengine wako kwenye uchunguzi.

“Haya yote yamefanikiwa kwa kuwa tumeimarisha sana kitengo cha ulinzi cha shirika kwa kuhakikisha wana fedha za kutosha," alisema.

"Tumepata wataalamu wenye uwezo mkubwa, wenye uwezo wa upelelezi (katika mikoa) ambao walikuwepo lakini hawakutumika ipasavyo.

“Kwa ujumla wake mikakati yote imewezesha shirika kuwa na mfumo ambao matumizi yake yote yanakuwa ni chini ya makusanyo na hivyo kuwa na uwiano mzuri kati ya mapato na matumizi.”

WAKURUGENZI SITA
Katikati ya mwaka jana, ikiwa ni miezi mitano baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF ambaye kwa sasa ni balozi, Dk. Ramadhani Dau, bodi ya shirika hilo ilifumua ungozi kwa kuwasimamisha kazi wakurugenzi wote sita wa idara kutokana tuhuma za ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya ofisi.

Mbali na wakurugenzi hao, bodi hiyo iliyokaa Julai 15 mwaka jana pia iliwasimamisha mameneja watano na mhandisi mmoja.

Taarifa ya NSSF kwa vyombo vya habari ilisema tuhuma nyingine zilizowakabili wakuu hao ni kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi na manunuzi ya ardhi, na ajira.

Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa bodi ya wadhamini wa shirika hilo ikiongozwa na Mwenyekiti Profesa Samwel Wangwe ilifikia maamuzi ya kuwasimamisha viongozi hao baada ya kupitia taarifa mbalimbali za wakaguzi wa mahesabu na shughuli za uendeshaji wa NSSF.

Uchunguzi huo bado unaendelea katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa mujibu wa taarifa za nyakati mbalimbali za maofisa wake.

Waliosimamishwa ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na miradi, Yacoub Kidula, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha, Ludocick Mrosso na aliyekuwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Chiku Matessa.

Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Udhibiti Hasara na Majanga, Sadi Shemliwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani, Pauline Mtunda na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji, Crescentius Magori.

Mameneja waliosimamishwa, kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni Meneja wa Utawala, Amina Abdallah, Meneja wa Uwekezaji, Abdallah Mseli na Meneja wa Miradi, Mhandisi John Msemo.

Wengine ni aliyekuwa Mhasibu Mkuu, Davis Kalanje, Meneja Kiongozi kwa mkoa wa Temeke, Wakili Chedrick Komba na aliyekuwa Meneja Mradi, mhandisi John Ndazi.

Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa NSSF, Ramadhan Dau Februari 16.

Utenguzi wa Dau ulikuja siku chache baada ya taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuonyesha palikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika miradi kadhaa ya NSSF.

Habari Kubwa