NSSF yaboresha huduma kiganjani

09Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
SIMIYU
Nipashe
NSSF yaboresha huduma kiganjani

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limesema kuwa limefanya maboresho ya uandikishaji na uchangiaji kwa wanachama wake, ambao kuanzia sasa utafanyika kwa wanachama wenye vitambulisho vya taifa.

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof.Florens Luoga, akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Sekta isiyo rasmi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), John Mwalisu (kulia) kuhusu shughuli Shirika hilo, alipotembelea banda la NSSF katika maonesho ya Wakuliama- Nanenane, yanayoendelea viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu. Kulia ni Kaimu Meneja wa NSSF mkoani Simiyu, Nuhu Mmbaga (Picha: Mpiga PIcha Wetu, SIMIYU)

Aidha, uandikishaji wa wanachama kwa muundo huo utasaidia kurahisisha huduma na kuokoa muda.

Meneja wa Sekta isiyo rasmi wa NSSF, John Mwalisu, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Alisema kupitia kitambulisho cha Taifa, Shirika linapata taarifa zote muhimu za mwanachama na kurahisisha usajili.

Kwa mujibu wa Mwalisu, NSSF imewarahisishia mwanachama kwa kuwa sasa wanachangia kupitia simu ya mkononi popote walipo baada ya kupewa namba ya kumbukumbu kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa malipo Serikalini (GePG) .

Alisema uchangiaji kupitia simu ya mkononi umeongeza ufanisi na viwango vya kuchangia vimeongezeka, na kuondoa usumbufu wa mwanachama waliolazimika kwenda ofisi za NSSF.

Meneja huo alibainisha kuwa kiwango kinachotakiwa kuchangiwa na mwanachama wa sekta isiyo rasmi kwa mwezi ni kuanzia Sh. 20,000.

Kwa mujibu wa Mwalisu, mwanachama anaweza kuona michango yake kupitia simu ya mkononi ama kwa kupakua “Application ya NSSF Taarifa inayopatikana kwenye Google Play Store.”

Nao baadhi ya wajasiriamali walioshiriki maonyesho hayo, Joash Omeme, alisema baada ya kupewa elimu na maofisa wa NSSF aliamua kujiunga na kupatiwa kadi ya uanachama papo hapo.

Aidha, aliwashauri wajasiriamali wenzake kujiunga na NSSF ili waweze kufaidika na mafao mbalimbali ikiwemo mafao ya uzeeni, mafao ya uzazi pamoja na mikopo ya kuinua biashara zao.

Naye, Peter Chacha, mkazi wa Mwanza, aliwashauri wajasiriamali wadogo kujiunga na NSSF kwa kuwa ni sehemu salama kwa wajasiriamali, wakulima na wavuvi.

Habari Kubwa