Nyalandu awashukuru, akana taarifa za whatsApp

01Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Nyalandu awashukuru, akana taarifa za whatsApp

Siku chache baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujivua Ubunge na pamoja na nafasi nyingine ndani ya chama hicho, amewashukuru watu wote waliompongeza na kumuunga mkono kwa maamuzi yake aliyochukua ya kujiondoa ndani ya chama hicho.

Lazaro Nyalandu.

Nyalandu ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook kwa kuandika hoja zilizopo mbele kwa sasa ni kubwa kuliko mtu mmoja mmoja na zinalenga kuleta utashi kwa kila Mtanzania kutafakari na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuendeleza nchi katika Demokrasia, Uchumi na kijamii.

"Nachukua nafasi hii kumshukuru kila mmoja wetu ayenitumia salaam na kuunga mkono hatua niliyochukua. Hoja zilizombele yetu ni kubwa kuliko mtu binafsi mmoja mmoja, na zinalenga kuhuisha utashi wa kila Mtanzania kutafakari na kushiriki kikamilifu safari ya kuiendeleza nchi yetu Kidemokrasia, kiuchumi, na kijamii.

 

 

Ameongeza kuwa "Ni maombi yangu kuwa, ujasiri ukaondoe roho ya woga, upendo uondoe chuki, nia njema iondoe kuoneana, na kweli ituweke huru na iondoe roho ya kusingiziana kunakoleta kuumizana na sintofahamu ya hali ya juu. Ikawe Heri kwa Watanzania wote" ameandika Nyalandu

Katika hatua nyingine Nyalandu amekanusha taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha alikuwa akiwasiliana kupitia kundi la Whatsapp na baadhi ya viongozi wa CHADEMA akionyesha hofu ya kushitakiwa na serikali kwa kosa la kuuza vitalu kipindi akiwa Waziri wa Maliasili na kusema huo ni uzushi wa kutungwa na kusema hizo ni siasa za kizamani.

Habari Kubwa