Nyalandu azua mnyukano mitandao ya kijamii

03Nov 2017
Joseph Mwendapole
Nipashe
Nyalandu azua mnyukano mitandao ya kijamii

MJADALA kuhusu hatua ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, kukihama chama chake umeendelea kupamba moto na kusababisha mnyukano kwenye mitandao ya kijamii; kwa watu kufanya majibizano.

Lazaro Nyalandu.

Wanaojibizana kwenye mitandao hiyo ya kijamii, ikiwamo WhatsApp, ni wale wanaoonekana kuwa makada na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wafuasi wa Chadema na wengine wenye mwelekeo wa uanaharakati ambao wanaonekana kuunga mkono uamuzi wa Nyalandu kukihama chama hicho.

Baadhi ya wanaoonekana kuiunga mkono CCM wamekuwa wakirusha maneno ya kumdhihaki Nyalandu na kumwonyesha kama mtu ambaye alikuwa amechokwa ndani ya chama hicho, hivyo kuondoka kwake hakuna athari kwa kuwa ilikuwa atimuliwe.

Wanaomuunga mkono wamekuwa wakiwajibu wenzao kuwa kama alikuwa mzigo ilikuwaje akadumu kwenye chama hicho hadi pale alipotangaza kukihama. Nyalandu alikuwa Mbunge wa CCM tangu mwaka 2000.

Mmoja wa wanaounga mkono hatua ya Nyalandu kuihama CCM aliweka picha ya Nyalandu kwenye ukurasa wake wa Twitter ikionyesha mwansiasa huyo akinadiwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2015, kisha akahoji "hivi hapo alikuwa hajaanza kuuza twiga?"

Watu wanaomponda Nyalandu kwenye mitandao hiyo, pamoja na kashfa nyingine, wanadai alihusika kuuza twiga waliosafirishwa kwenda ughaibuni akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mtumiaji huyo wa Twitter alihoji kama ubaya wa Nyalandu umekuja baada ya yeye kudai katiba mpya.

Mwingine aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Facebook alisema ni CCM iliyokuwa ikimpitisha kugombea ubunge kwa vipindi vinne.

Aliyejibu ujumbe huo aliandika kuwa Nyalandu alipitishwa na chama kilichokuwa na viongozi wengine na si hawa wa awamu ya tano ambao hawavumilii watu wenye kashfa.

Kada maarufu wa CCM na Mbunge wa Jimbo la Mtera mkoani Dodoma alituma ujumbe wa ‘video’ ukiwasihi Watanzania wapuuze madai ya Nyalandu kuwa Serikali inaikandamiza CCM na kupoteza mwelekeo.

Lusinde anasikika kwenye ‘video’ hiyo akisema Nyalandu aliyemuita mwenye bahati, hakuwahi kunyimwa nafasi yoyote ya kutoa maoni yake ama dukuduku zake ndani ya chama wala bungeni na kwamba uamuzi huo unaashiria kuwa anatafuta kinga ya kutochukuliwa hatua kutokana na tuhuma nzito zinazomkabili.

Lusinde alijibiwa na mmoja wa watu wanaoonekana kumuunga mkono Nyalandu kuwa kitu pekee anachomzidi mwanasiasa mwenzake huyo ni matusi na anapaswa kurudi nyuma kuangalia historia ya maisha yake kisha ajiulize nani mwenye bahati kati yao.

"Nyalandu na Lusinde wasingekutana bungeni mwaka 2010 huenda leo Lusinde angekuwa anamsalimia Nyalandu shikamoo baba hata kama wamepishana miaka miwili tu ya kuzaliwa," alisema mchangiaji huyo.

KUNDI MOJA
Mpambano mwingine ulitokea kwenye kundi moja la WhatsApp la waandishi wa habari ambapo baadhi walikuwa wakihoji iweje taarifa ya Bunge kuhusu kufutwa kwa ubunge wa Nyalandu iingiza maoni ya CCM.

"Usipoteze nguvu nyingi kujadili jambo ambalo hufaidiki nalo cha msingi fahamu kwamba Nyalandu hayuko CCM tena yuko Chadema. Kauli hizi zisikufanye utumie nguvu kubwa maana wewe mara nyingi unaongozwa na mihemko ya kichadema chadema tu," aliandika mmoja wa wachangiaji kwenye kundi hilo.

Mchangiaji mwingine aliandika kuwa kwenye kundi hilo kuna watu wasiostahili kuwemo na kuwataka waende kwenye makundi mengine ya propaganda za vyama badala ya kuwa kwenye kundi la kitaaluma kama hilo.

"Nendeni kwenye kundi la wanasiasa mkajadili masuala ya Nyalandu na masuala mengine ya siasa kundi hili tuachieni sisi wanataaluma," aliandika mchangiaji huyo wa kundi la waandishi wa habari.

Taarifa ya Bunge juzi ilisema kuwa haijapokea barua ya Nyalandu kujiuzulu, lakini imepokea barua ya Katibu Mkuu wa CCM, inayoelezea kuwa Nyalandu si mwanachama tena wa chama hicho hivyo si mbunge tena.

Nyalandu alitangaza kujivua gamba CCM, kuandika barua ya kuachia kiti cha ubunge na kueleza nia yake ya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jumatatu iliyopita.

Chadema, kupitia Katibu Mkuu wake, Dk. Vicent Mashinji, kilitangaza kumpokea awe mwanachama na kwamba alichelewa kutoa uamuzi huo.

Katika taarifa yake ya kujitoa CCM Nyalandu aliyochapisha katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, Nyalandu aliomba kutua Chadema ili aungane nao kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini.

"Nitaomba kama itawapendeza wanachama wa Chadema, basi waniruhusu kuingia mlangoni mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na Chadema na Watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa kidemokrasia na uhuru wa mawazo."

Nyalandu (45) alisema amejiuzulu ubunge kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine, ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na changamoto lukuki.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida na Mjumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, alisema: "Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, sote kama taifa tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu."

Aliandika zaidi: "Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa haki itamalaki Tanzania, upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za kisiasa na makabila yote nchini uimarike. Tushindane kisera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu na taifa lililo imara na nchi yenye adili."

Nyalandu alitangaza nia kuwania urais Desemba 28, 2014 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Ilongero jimboni kwake, wakati akihutubia mamia ya wananchi.

Katika mkutano huo, Nyalandu alisisitiza "sasa ni zamu ya vijana kuongoza nchi" huku akiwaambia wananchi kuwa safari yake ya ubunge kwa miaka 15 inaanzisha safari nyingine bila kuwaeleza ikiwa bado ana nia na ubunge au la. Siku hiyo, aliambatana na mkewe, watoto na wazazi wake.

Ingawa alikuwa mmoja kati ya wanaCCM 38 waliojitokeza kuwania urais mwaka 2015, jina lake lilikatwa pamoja na kina Lowassa na Sumaye na kuteuliwa Rais Magufuli kupeperusha bendera ya chama hicho.

Habari Kubwa