Nzige waleta hofu kwa wananchi Longido

21Feb 2021
Zanura Mollel
Longido
Nipashe Jumapili
Nzige waleta hofu kwa wananchi Longido

MAKUNDI ya Nzige yaliyovamia vijiji vilivyopo Kata ya Kimokouwa katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha, yameanza kuleta hofu ya baa la njaa na kusababisha hasara kwa wakulima waliopanda mazao ya chakula na biashara karibu na mpaka wa Namanga.

Jana, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, alithibitisha kuwapo kwa makundi Nzige kuhama vijiji kwa vijiji kuelekea mpakani na wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.

"Nzige walionekana kwa mara ya kwanza juzi jioni katika mpaka wa Namanga unaozitenganisha nchi za Kenya na Tanzania, wameshaingia Kijiji cha Eworendeke na Kimokouwa vilivyopo Kata ya Kimokouwa, Wilaya yetu ya Longido,” alisema na kuongeza:

"Wameshaanza kula majani na matawi ya miti, lakini kuvamia maeneo ya kilimo bado sijapata taarifa za uharibifu isipokuwa wakulima wengi wa Wilaya yetu wapo ukanda wa West Kilimanjaro (Siha),”alibainisha.

"Kwa sasa wameingia eneo la wanyamapori , tumeshawasiliana na wataalamu wa Wizara ya Kilimo nao wamesema wanawasiliana na wataalamu wao wa Kanda ya Kaskazini. Hivyo muda si mfupi tutapata msaada."

Akizungumzia uvamizi wa Nzige hao, Diwani wa Kata ya Kimokouwa, Solomon Kool, alisema hivi sasa pia jamii za wafugaji nazo zinahofia kupotea kwa maeneo ya malisho kutokana na kundi la nzige hao.

"Nzige hawa walitokea eneo la Orkong'u upande wa mpaka wa Kenya kuingia Tanzania. Wamegawanyika katika makundi mawili, kuna kundi lililoelekea upande wa Sinya, Tarafa ya Enduiment na lingine ndiyo hili lilikobaki hapa Kitongoji cha Sikarida " alifafanua Kool.

Kwa mujibu wa Kool, kundi kubwa la nzige lilivamia Kijiji cha Eworendeke na kushambulia zaidi ya hekari 40 za malisho ya mifugo.

Alisema wakazi wa kata hiyo asilimia 95 wanajishughulisha na ufugaji na uhifadhi huku asilimia tano akijishughulisha na kilimo cha mahindi, magharage, nyanya na vitungu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Eworendeke, Lomayan Ole Sambau, alisema ameshafanya mawasiliano na vijiji vinavyopakana na kitongoji hicho ili nzige hao wanapooneka watoe taarifa na kupata msaada wa kudhibitiwa.