Ofisa Uhamiaji matatani kwa kuomba na kupokea rushwa

12Dec 2019
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Ofisa Uhamiaji matatani kwa kuomba na kupokea rushwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilayani Kahama mkoani Shinyanga imemtia hatia Ofisa Uhamiaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume cha sheria.

Ofisa huyo Cosmas Ntakisigiye Eliud ametiwa hatiani kwa kutenda kosa hilo kinyume cha sheria kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha sheria ya kuzia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2017.

Cosmas awali alishitakiwa katika kesi ya jinai namba 147/208 katika mahakama ya wilaya ya kahama kwa kosa la kuomba rushwa kiasi cha shilingi laki tatu kutoka kwa Bosile Chacha kama kishawishi cha kutochukua hatua juu yake aliyekuwa na mashitaka ya uraia wake.

Kiasi cha fedha alichoomba Ofisa huyo kutoka kwa mshitakiwa Busile Chacha ni Tsh. 100,000 kwa lengo la kutokumchukulia hatua za kisheria.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama Evodia Kyaruzi alimtia hatiani Ofisa huyo kwa kosa la kujipatia kiasi cha shilingi laki moja kutoka kwa mtuhumiwa.

Hakimu Kyaruzi alimtaka mshitakiwa huyo ambae ni Ofisa Uhamiaji kwenda jera miaka mitatu au kulipa faini kiasi cha shilingi laki tano(500,000).

Aidha Kyaruzi aliwataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kama ambavyo wamekuwa wakifanya ili kuondoa kero ya rushwa katika mkoa wa shinyanga.

Habari Kubwa