Ofisa ardhi mbaroni kwa  tuhuma kughushi nyaraka 

13Jan 2018
Rose Jacob
Nipashe
Ofisa ardhi mbaroni kwa  tuhuma kughushi nyaraka 

WATU  watano, akiwamo Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Ilemela, Alloyce Nyabange,  wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za utapeli wa kuuza viwanja kwa kutumia nyaraka za kughushi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema mbali na Nyabange, watuhumiwa wengine ni Alex Josephat (41) mfanyabiashara na mkazi wa mtaa wa Buswelu, Juma Malulu (60) mkazi wa mtaa wa Ilemela ambaye ni mkulima, Getruda Kokuberwa (42) mkazi wa mtaa wa Nyegezi na katibu muhtasi wa ofisi iitwayo Nyambale Civil Works na Deodatus Musinyi (51) mchora ramani za viwanja mkazi wa mtaa wa Usagara.

Msangi alisema Desemba 30, mwaka huu,  majira ya saa 08:15 mchana maeneo ya Buswelu, wilaya ya Ilemela, watuhumiwa hao wa utapeli wa kuuza viwanja viwili vilivyopo eneo la Nyasaka wilayani humo, wanadaiwa  kutumia nyaraka za kughushi kwa Sh. milioni 45 kutoka kwa Barnabas Nibengo kisha kupewa fedha za kianzio kiasi cha Sh. millioni sita.

“Matapeli hao walifika kwa Nibengo na kuongea naye juu ya kumuuzia viwanja vilivyoko mtaa wa Nyasaka. Baadaye alikubali kununua viwanja vyote viwili kwa Sh. milioni 45  na inadaiwa kuwa baada ya maelewano watuhumiwa hao walimwomba mnunuzi awape Sh. milioni 10 kama kianzio na fedha zingine atamaliza baadaye lakini mnunuaji hakuwa na fedha hizo wakati huo hivyo aliwapa Sh. milioni sita tu,” alisema Msangi.

Alisema baada ya kulipa fedha, Nibengo alikwenda kwa mwenyekiti wa mtaa wa eneo analotaka kununua ili kujua umiliki halali wa watu hao katika eneo hilo na kuelezwa kuwa watu hao ni matapeli hawana viwanja katika eneo hilo. 

Kamanda Msangi alisema baada ya kupata ukweli wa jambo hilo, Nyabengo alitoa taarifa polisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, baada ya kupokea taarifa hizo, polisi walifuatilia haraka na kuwakamata watuhumiwa watano na kufanya upekuzi katika makazi yao na kukuta hati feki mbili za viwanja zenye muhuri wa moto, ‘tape measure’ moja  yenye urefu wa mita 100 na ‘CPU’ moja  iliyokuwa ikiweka kumbukumbu. 

Kutokana na kuwakamata watu hao, Msangi alisema polisi wanawahoji watuhumiwa wote na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika. Pia alisema wanamtafuta  mtuhumiwa mmoja ambaye bado hajapatikana.