Ofisa NIDA mbaroni tuhuma kutoza fedha utoaji namba ya kitambulisho

20Jan 2020
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Ofisa NIDA mbaroni tuhuma kutoza fedha utoaji namba ya kitambulisho

OFISA Msajili Msaidizi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mkoani Shinyanga Haroon Mushi, pamoja na wakala wa usajili laini za simu za mkononi  Victor Vicent, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoza fedha wananchi Shilingi 30,000, ili wawapatie namba za Nida.

Ofisa usajili msaidizi wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa Nida mkoani Shinyanga Haroon Mushi katikati akiwa mkononi mwa Polisi.

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa saba mchana wakati Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, alipofika kwenye ofisi za  mamlaka hiyo na kupata taarifa hizo za wananchi kuombwa fedha ili wapate namba za Nida ili wakasajili laini zao za simu kwa alama za vidole.

Akielezea tukio hilo mkuu huyo wa wilaya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Shinyanga, amesema wakati akiwa kwenye ofisi hizo za Nida, akapata taarifa hizo za uombwaji fedha wananchi kutoka kwa wakala wa usajili wa laini za simu za mkononi ambaye alikuwa akifanya mawasiliano na ofisa huyo wa Nida.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza na wananchi kuacha tabia ya kutoa fedha ili wapate namba za vitambulisho vya taifa Nida. Amesema namba hizo zinatolewa bure na kuwataka wananchi wawe wavumilivu hata kama laini zao zitazimwa bali zoezi hilo litaendelea na watapatiwa namba wakasajili laini zao kwa alama za vidole.

Amesema mara baada ya kumkamata wakala huyo , walipomfikisha Polisi na kuanza kumhoji kwanini anatoza fedha wananchi ili awapatie namba za Nida, na wakati yeye siyo mtumishi wa Nida, ndipo akasema hua ana shilikiana na mmoja wa maofisa na Nida.

“Baada ya kumkamata wakala huyu wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama za vidole, ndipo akamtaja Ofisa huyu wa Nida Haroon Mushi kuwa wanashilikiana naye kuomba fedha wananchi, ambapo yeye ndio mtoaji wa namba za Nida, na wakala huyu wa simu ndio mkusanyaji wa fedha,” amesema Mboneko na kuongeza kuwa;

“Tulipopewa taarifa hiyo ikabidi tumkamate na huyu Ofisa wa Nida Haroon Mushi, ambapo tumefanya uchunguzi wa simu zao na kubaini kuwapo na mawasiliano ya wananchi kuwaomba fedha na baadhi yao wameshatuma fedha hizo kwenye simu zao, ambapo bado tunaendelea na uchunguzi zaidi,”

Ofisa Msaidizi Msajili wa NIDA mkoani Shinyanga Haroon Mushi kushoto akiwa na wakala wa usajili laini za simu za mkononi Victor Vicent kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Shinyanga.

Pia ametoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kuacha tabia ya kutoa fedha ili kupata namba za vitambulisho hivyo vya taifa Nida, ikiwa Serikali inatoa namba hizo bure, huku akiagiza maofisa wa Nida wafanye kazi usiku kucha na kutofunga ofisi hizo, hadi pale watakapo wamaliza watu wote kuwapatia namba hizo za Nida.

Kwa upande mtuhumiwa huyo Vicent, amekiri kufanya kazi hiyo ya kuomba fedha wananchi  ili awasaidie kupata namba za Nida, kwa kushirikiana na ofisa huyo wa Nida, Haroon Mushi, huku akiomba msamaha kwa kufanya makosa hayo.

Naye Mushi, amekanusha tuhuma hizo za kushirikiana na wakala huyo wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama ya vidole kuomba fedha wananchi, huku akikiri hua anampatia majina ya watu kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi na kisha kumuangalizia namba za Nida.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Joseph Paulo, amethibitisha kuwatia mbaroni watu wawili ambaye mmoja ni ofisa wa Nida na Wakala wa usajili wa laini za simu za mkononi, na kubainisha kuwa upelelezi bado unaendelea ambapo wamewakabidhi Takukuru na  ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Baadhi ya wananchi mkoani Shinyanga wakiwa kwenye ofisi za Nida Shinyanga mjini wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akiwa tahadharisha kuacha kutoa fedha ili kupata namba hizo. PICHA ZOTE NA MARCO MADUHU

Habari Kubwa